Arusha.
Mamia ya wafuasi
wa Chadema jana, waliandamana katikati ya jiji, wakati mvua ikinyesha
wakimtembeza Diwani mpya wa Kata ya Sombetini, Ally Benanga huku,
viongozi wakitoa kauli kuwa siku za Meya wa Jiji la Arusha, Gaudence
Lymo kukaa madarakani zinahesabika.
Mamia ya wafuasi hao, wakiongozwa na mbunge wa
Jimbo la Arusha, Godbless Lema,aliyekuwa kwenye gari la wazi la Benanga,
bila kujali mvua waliandamana kutoka ofisi za chama hicho hadi Jiji la
Arusha kwa kupita barabara za Sokoine na baadaye kurejea katika ofisi za
chama hicho, eneo la Ngarenaro.
Hata hivyo, ingawa maandamano hayo, yalikuwa
hayana kibali, polisi walilazimika kuyasindikiza ili kuepusha vurugu
kubwa na hakuna vurugu ambayo ilitokea.
Watangaza kumng’oa Meya
Akizungumza mara baada ya maandamano hayo,
Mwenyekiti wa Vijana wa Chadema Mkoa wa Arusha,, Ephata Nanyaro, ambaye
pia ni Diwani wa Kata ya Levolosi, alisema baada ya kupata ushindi wa
Kata ya Sombetini, kazi ambayo ipo mbele yao ni kumng’oa Meya kwani wana
idadi ya kutosha kuongoza jiji kwa sasa.
“Tayari tumeandaa tuhuma zake na tutapeleka jiji
kuomba kikao maalum cha Baraza la Madiwani ambacho kitakuwa na ajenda
moja tu juu ya utendaji wa Meya”alisema Nanyaro.
Alisema kikao hicho, kitakuwa cha wazi na akaomba
wakazi wa jiji, kujitokeza wakipata taarifa kwani, tuhuma ambazo
watatumia kumng’oa Meya Lymo zipo wazi .
Naye Lema akizungumza na mamia ya wakazi wa Jiji
la Arusha, aliwapongeza kwa kumchagua diwani wa Chadema Kata ya Sombetni
na sasa kufanya Chadema kuwa na jumla ya madiwani pamoja na wabunge 16
katika jiji la Arusha..
“Kuanzia sasa sisi ndiyo tutaongoza Jiji,
tunawahakikishia tutashughulikia matatizo yenu ya ukosefu wa huduma bora
za afya, barabara, viwanja, elimu na nyingine i”alisema Lema.
Alisema hivi sasa Jiji lina mpango wa kugawa
viwanja na watakaonufaika ni watu kawaida walio na shida ya ardhi na
siyo viongozi kama ambavyo imezoeleka kwa kuwa kamati ya mipango miji
sasa itakuwa chini ya uongozi na usimamizi wa Chadema.
No comments:
Post a Comment