Wajumbe wanawake wa Bunge Maalumu la Katiba na wageni wa jinsi
hiyo watakaovaa nguo fupi ‘vimini’ au nguo za kubana, hawataruhusiwa
kuingia ndani ya Ukumbi wa Bunge.
Hayo yamo katika mapendekezo ya rasimu ya kanuni
za uendeshaji wa Bunge hilo, zilizowasilishwa katika semina mahsusi ya
kupokea rasimu hizo, iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati Maalumu,
Profesa Costa Mahalu.
Kanuni ya 82 (9) ya mapendekezo hayo imeainisha
vazi rasmi linaloruhusiwa kuwa ni vazi lolote la heshima ambalo siyo la
kubana mwili, lisiloonyesha maungo.
Pia imeainisha mavazi yanayoruhusiwa kwa wanawake
kuwa ni pamoja na gauni la kitenge au blauzi inayovaliwa na kitenge au
sketi ya rangi yoyote, suti ya kike, vazi linalovaliwa wakati wa eda na
kilemba cha kadri au mtandio.
Kwa upande wa wanaume, mavazi rasmi ni suti ya
Kiafrika au safari ya mikono mirefu au mifupi yenye ukosi au shingo ya
mviringo na fulana.
Kulingana na kanuni hiyo, upande wa wanaume, pia
imeainisha vazi rasmi kwa jinsia hiyo kuwa ni suti ya Kimagharibi, shati
na tai, suruali ya aina yoyote isipokuwa suruali aina ya ‘jeans’.
Sehemu ya 6 ya kanuni hiyo, imeweka wazi kuwa
mjumbe yeyote wa Bunge Maalumu, anaweza kutoa taarifa kwenye Bunge au
kwenye kamati iwapo mjumbe mwingine ataingia akiwa amevaa vazi
linalovunja au kukiuka masharti ya kanuni.
“Mwenyekiti wa Bunge Maalum au mwenyekiti wa
kamati maalumu atakaporidhika kuwa mjumbe huyo aliyetolewa taarifa
hajavaa vazi rasmi, atamwamuru atoke nje ya ukumbi wa mikutano wa
kamati,” inaseme sehemu ya kanuni hizo.
Kwa mujibu wa kanuni hiyo, mjumbe aliyeamriwa
kutoka nje ya ukumbi, hataruhusiwa kuingia tena hadi pale atakapokwa
amevaa mavazi rasmi.
Wakati huohuo, kamati hiyo imependekeza Bunge hilo liwe na kamati 16.
Akiwasilisha taarifa ya kamati hiyo jana katika
semina ya wajumbe wa Bunge hilo, Mwenyekiti wake, Profesa Costa Mahalu,
alizitaja kamati hizo kuwa ni Kamati ya Uongozi ya Bunge Maalumu.
Zingine; Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge Maalumu, Kamati ya Uandishi, Kamati ya Maridhiano na Kamati nyingine 12.
“Kwa mpangilio huo, jumla ya kamati zote za Bunge Maalumu
zinazopendekezwa na kamati hii ni 16 na majukumu ya kila kamati
yameelezwa katika sehemu hiyo,” alisema Profesa Mahalu.
Profesa Mahalu alisema kamati yake haikufanyia
marekebisho sehemu ya saba ya rasimu ya kanuni za Bunge Maalumu
inayoweka utaratibu wa jinsi ya kutunga masharti ya mpito na yatokanayo.
Alisema katika sehemu ya tisa, kamati yake
imependekeza kanuni mpya inayoruhusu Rais wa Jamhuri ya Muungano, Rais
wa Zanzibar au Rais wa nchi nyingine yoyote kutambuliwa kama wageni.
No comments:
Post a Comment