Moshi.
Jeshi la Polisi limewafukuza chuo wanafunzi wa mafunzo ya uaskari 212 wa Chuo Cha Taaluma Moshi baada ya wanafunzi hao kubainika kughushi vyeti vya elimu ya sekondari.
Kamishna wa Utawala na Utumishi kutoka jeshi la
polisi, Thobias Andengenye ametoa taarifa hizo jana wakati wa kikao cha
waandishi wa habari na maofisa wa polisi kilichofanyika chuoni hapo
kilichopo Moshi mkoani Kilimanjaro.
CP Andengenye alisema uamuzi wa kuwafukuza chuo
wanafunzi hao umekuja baada ya jeshi hilo kwa kushirikiana na baraza la
mitihani la taifa kubaini vyeti vya wanafunzi 212 kati ya 3,390 kuwa
vimeghushiwa.
Alisema jumla ya wanafunzi 3,415 waliripoti chuoni
na kati yao 25 walishindwa kuendelea na masomo kutokana na sababu
mbalimbali ikiwamo ya utovu wa nidhamu na matatizo ya kiafya.
“Baada ya hawa 25 kuondoka tulipeleka majina
kwenye baraza ili kuhakiki vyeti na baraza la mitihani limetuletea
majibu wiki iliyopita na kubaini vyeti vya wanafunzi wa uaskari 212 ni
vya kughushi,”alisema Andengenye.
Alisema jeshi hilo linaendelea na hatua za
upelelezi kwa kushirikiana na taasisi nyingine ili kujua wanaohusika
kuwaghushia vyeti hivyo.
“Itambulike kuwa kitendo cha kughushi ni kosa la
jinai na pindi unapobainika polisi haitasita kuwachukulia hatua za
kisheria,” alisema Andengenye.
Hata hivyo amewataka wananchi kuacha tabia za
kughushi vyeti na badala yake wafuate sheria na taratibu zilizopo kwa
ustawi wa taifa.
Wanafunzi hao walianza mafunzo ya uaskari Disemba mwaka jana ambapo walitarajia kumaliza mafunzo ya awali Septemba mwaka huu.
Tatizo la kughushi vyeti nchini limekuwa sugu hususani katika idara mbalimbali zikiwamo polisi, uuguzi ,ualimu na nyinginezo
No comments:
Post a Comment