Saturday 10 May 2014

‘MALEZI;Wazazi wapya’ na malezi ya ‘pampas’ na mitandao

KULEA mtoto mchanga ni kazi nzito yenye changamoto nyingi hasa pale unapohitajika na dunia kumkuza mtu, ambaye atachangia katika ustawi wa dunia hii. Changamoto inakuwa kubwa zaidi kwa sababu hakuna maelekezo ya malezi yanayokidhi mahitaji ya wakati wote au mazingira yote.

Walivyolea wazazi wetu ni tofauti na tunavyolea kwa sasa. Lakini mwisho wa siku kiumbe anayelelewa anatakiwa kuwa na tabia inayokubalika na jamii inayomzunguka na dunia kwa ujumla. Hivyo tofauti za malezi hazina matatizo kama zote zinalenga katika kumkuza mtu wa namna hiyo.

 Leo ningependa tutafakari malezi yatolewayo na wazazi wapya, siyo kwa sababu nataka walee kama sisi lah, naamini hilo haliwezekani. Pia siyo kwamba malezi yetu yalikuwa bora sana kwani tuna watoto wenye tabia mbaya sana, hivyo nasi kuna sehemu tulishindwa. Napenda tuzungumzie masuala kadhaa ambayo mimi naona kama yataendelea yatachangia katika kuhatarisha usalama wa watoto na kuwajengea tabia za uchafu na kukosa ukatili.

Kwanza ni matumizi ya nguo za kumsitiri mtoto katika haja kubwa na ndogo na athari yake kitabia. Wakati wetu sisi tulikuwa tunatumia nepi kwa walionazo na vitambaa vya khanga zilizochakaa kwa wasionazo. Hizi zote zilihitajika kufuliwa. Hivyo kila ikichafuka mtu alikuwa analazimika kufua. Kwa sasa kuna mabadiliko kwani zipo ‘pampas’ kwa kazi hiyo ila tofauti ni kwamba zenyewe hazifuliwi bali hutupwa baada ya matumizi.

Kwa maana hiyo wazazi wenye kulea kichanga wanahijika kuwa nazo za kutosha.  Sina tatizo na matumizi ya pampas kwani hata zingekuwepo wakati wangu nami ningezitumia kwani zinapunguza muda mrefu unaotumika kufua nepi na karaha nyinginezo ziletwazo na uhitaji wa kufua nepi.

Ugomvi wangu unakuja kwa wazazi wapya wasio na uwezo wa kununua pampas za kutosha na wasio na mfumo mzuri wa kuziondoa, usioharibu mazingira, nao kujilazimisha kutumia pampas.

Kwa ajili ya uwezo mdogo wa kununua pampas za kutosha, mama au baba analazimika kumvisha mwanaye pampas moja kwa muda mrefu, sana akijisaidia mara kadhaa kwenye pampas hiyo matokeo yake ni mtoto kukaa na ubichi muda mrefu, ambao kama binadamu unamkosesha raha, unamchubua na kibaya zaidi ni kwamba unamjengea TABIA YA UCHAFU.

Wazazi wapya hebu wafikirieni wale makondakta wa daladala ambao wakikukaribia tu ni harufu ya uvundo wa nguo zao za ndani, wafikirieni wale wasusi ambao wakisema tu “geukia kwangu” mnasikia kichefuchefu kwani kwao inatoka harufu mbaya sana ya nguo zao za ndani,  sasa tabia hiyo ndiyo mnayowajengea watoto wenu msiowabadilisha pampas pale wanapoenda haja.

 Kukaa na uchafu itakuwa ni kawaida. Tukiacha hao watoto wenu hata sisi mnatukera. Pampas zinakuwa zimetota na haja za watoto wenu kiasi kwamba hazichomeki na suluhisho kwenu ni kuzitupa popote. Angalia jinsi zinavyochafua mazingira. zikishindana na mifuko ya plastiki na afadhali kuangalia mifuko ya plastiki kuliko hizo haja za watoto wenu. Hakika mnatia aibu.

Jambo la pili ambalo ningependa tulitafakari ni tabia ya wazazi wapya kutegemea sana  vyombo vya habari za nje kuwapa namna ya kulea watoto wao.  Jambo moja ambalo wamelinukuu ama kwa uvivu walionao, wamama wengine au kwa kuona hiyo ni sahihi ni kuwaachia wasichana wa kazi malezi ya watoto kwa muda mrefu.

Mama anarudi kazini na kuishia kunyonyesha tu.  Yupo nyumbani wikiendi, sikukuu au likizo, lakini kama wanavyoonyeshwa kwenye televisheni mtoto wake mchanga ataogeshwa, atavishwa, atalishwa, atapakatwa au kulazwa na msichana wa kazi.

Kwa mtazamo wangu hali hii inaweza ikawa salama kwa mtoto kwa mazingira ya wazungu, lakini siyo salama kwa mazingira yetu. Wale walezi wanaowaona kwenye mitandao ni watu wazima wenye ujuzi na uzoefu wa kazi hiyo ya malezi hivyo watoto wana usalama.

Sasa angalia huku kwetu mlezi ni mdogo ki umri na hana ujuzi wala uzoefu wa kulea mtoto. Hajui kumshindilia mtoto chakula wakati analia kunaweza kusababisha kifo. Ukweli ni kwamba wana upungufu mwngi katika malezi ya watoto. Kwa kuwa walezi wetu wana upungufu inabidi watumike tu kuziba mapengo ya muda, ambao mama anakosekana katika ulezi huo.

Siwezi kusema kwa maisha ya leo mama awepo nyumbani masaa yote kwani naitambua hali mbaya ya kiuchumi, ambapo kumfanya mama akae muda wote nyumbani kunaweza kukamkosesha mama huyo hata lishe yake, ambayo inahitajika kwa ajili ya kutengeneza maziwa ya mtoto. Lakini bado nasisitiza umuhimu wa mama kuhakikisha anakuwa karibu na mtoto wake kila inapowezekana.

Mtu umerudi toka kazini, au upo likizo au ni mwisho wa juma hivyo upo nyumbani kwa nini usimwogeshe mwanao mwenyewe, hata ujue kama viungo vya mwili wake viko sawasawa? Pengine chakula unachokiacha mwanao hakipendi kabisa na kila siku anakula kidogo sana, kwa nini usimlishe mwenyewe upate kuling’amua hilo?

Pengine kabla ya kukurupuka na kuiga mtindo huu wa malezi tujiulize nini chanzo cha watoto wengine wa nje kukosa upendo na kuanza kuwafyatulia walimu na wenzao risasi.

Nani anajua, pengine ile kukosa  pendo la wazazi toka utotoni. Upendo wa wazazi huanzia mtoto akiwa tumboni na unapaswa uendelezwe katika kipindi chake cha utoto kwa kuwa karibu naye kipindi hicho. Upendo wa wazazi huchanua na kuwa upendo kwa watu wengine na hilo huanzia toka akiwa mdogo akiguswa na wazazi wake kwa kuogeshwa, kulishwa, kusemeshwa maneno mazuri

Atayapata wapi yote haya kama wazazi wote hawapo tena wakati mwingine kwa sababu hata zisizo na msingi. Eti wapo kwenye kumbi za starehe au wamekwenda kusalimia ndugu na jamaa baada ya kutoka kwenye mishughuliko. Hii siyo sahihi kama ilivyo si sahihi kwenda na watoto hao kwenye kumbi za starerehe. Wazazi wapya watoto wanawahitaji nyumbani tafuteni muda.

No comments:

Post a Comment