Tuesday, 27 May 2014

NI RAHISI SANA KUIMARISHA NDOA YAKO!

ILI uwe na ndoa yenye furaha ni lazima utenge muda wa kutafakari namna ya kuiboresha na kutafuta furaha ya ndoa hiyo. 

Waswahili wanasema, ukiona vyaelea, ujue vimeundwa. Huwezi kuacha mambo yakajiendesha hovyo ukategemea kuwa na ndoa bora. Uhusiano imara unakutegemea wewe.
Kila mmoja ana wajibu wa kuangalia furaha ya mwenzake. Yapo mambo mengi muhimu ambayo kama wanandoa wakiyafanya huboresha uhusiano wao, lakini hapa nitakutajia yale muhimu zaidi.

ISHI KIRAFIKI

Kuna baadhi ya wanandoa wakishaingia kwenye muunganiko huo, ule urafiki uliokuwa zamani wakati wa uchumba, hilo ni tatizo. Ukitaka kuwa na ndoa yenye furaha lazima umfanye mwenzi wako kama rafiki yako.
Baadhi ya wanaume wana tatizo la ubabe na kujiona kuwa wao ni wanaume hivyo hawapaswi kuguswa kwa lolote. Ndoa inageuka jeshini. Hilo ni tatizo.
Mshirikishe mwenzako kwenye mambo yako. Kuwa na kauli njema muda wote. Sikiliza shida za mwenzako na namna ya kuzitatua. Sikiliza pia hisia zake.
Usipoishi naye kirafiki, maana yake ataogopa hata kukueleza mambo fulani ya msingi ambayo labda havutiki nayo. Ukimsogeza kama rafiki atakueleza mambo ambayo hayamfurahishi.
Mkiishi kama marafiki ni rahisi kusameheana. Ndoa nzuri ni ile yenye kusameheana ndani yake. Kukaa na mambo moyoni husababisha mikwaruzano ya kudumu.
Kama marafiki, mtapata muda wa kushughulikia kero zenu haraka kabla hazijakua.

MIPANGO YA KIFEDHA

Kama kuna jambo linalosabisha migongano na kupunguza uaminifu ndani ya ndoa ni suala la fedha. Kwa bahati mbaya sana wanaume wengi ni wasiri sana kuhusu mapato yao.
Ndugu zangu, huna sababu ya kumficha mke wako kuhusu kipato chako. Mshirikishe, ajue unapata kiasi gani kwa mwezi. Labda una biashara nyingine au vyanzo mbalimbali vya mapato nje ya ajira yako ya kudumu, zungumza na mwenzako.
Ziko faida nyingi, kwanza ataona unavyomwamini na kumthamini na kumfanya sehemu ya mafanikio ya familia, lakini pia anaweza kukushauri mambo ya msingi ambayo yatasaidia kukuza kipato chenu.
Kubwa zaidi ni kwamba, utamfundisha namna ya kuendesha biashara zako, hata siku ikitokea umeugua atasaidia kuimarisha biashara. 

MATATIZO YA FAMILIA

Kuangalia matatizo ya pande zote mbili za familia mlizotoka, inasaidia kuimarisha mapenzi. Mwenzako akikuambia kuhusu tatizo labda la mtoto wa dada yake, usipuuze.
Hata kama hamna fedha, unaweza kumshauri jambo zuri ambalo litamuweka vizuri kihisia.

Wengine huwa na majibu mabaya: “Kwani nimekuoa wewe au ukoo mzima?” kauli hii siyo sahihi na hubomoa nyumba.

Kujua na kuthamini matatizo ya mwenzako ni kati ya mambo muhimu sana yanayoleta furaha kwenye ndoa. Kuwa na kauli nzuri. Kweli, inawezekana huna fedha au mipango yenu imeingiliana, isiwe tatizo.

Mjulishe mwenzako kwa lugha laini na ikiwezekana mawazo yako yanaweza kumfanya akajua mahali pa kuanzia. Kuchukulia tatizo la mwenzako kama lako, inaongeza amani, maana anajiona sehemu kamilifu ya muunganiko wenu wa ndoa.

Wengi hawajui hili na hata kama wanajua, hawatoi umuhimu mkubwa kwa wenzi wao. Ndoa ni tunu rafiki zangu. Tujitahidi kuheshimu na kuzilinda kwa nguvu zetu zote.

No comments:

Post a Comment