Thursday 10 July 2014

UNAISHI KWA MAZOEA? SHAURI YAKO!

HayaHAYA, tumekutana tena kupeana mawili matatu kuhusiana na maisha yetu ya kila siku. Kwa kweli wanawake kuishi kwa mazoea kumekuwa kukiongeza nyumba ndogo kila kukicha. Leo nataka nikupashe upashike kosa lako la kuishi kimazoea kumefanya mapenzi yapungue ndani ya nyumba nyingi.


Nyumba nyingi siku hizi zimepoteza mapenzi ya zamani kufikia hatua ya kuonana kaka na dada, kinachotofautisha ni makutano ya kimwili lakini zaidi ya hapo hakuna lolote linalofanya upendo kati yenu uonekane.


Tukio moja majuzi limenifanya nipanue mdomo wangu kwa nguvu zote ili niiondoe kutu hii iliyotanda ndani ya nyumba zenu.


Nikiwa nimemtembelea shoga yangu mmoja mkubwa kwa kweli, tokea nikiwa jirani yao wakati akiwa binti mdogo mpaka alipoolewa na kupata watoto watatu na ndoa yao ilikuwa inafika mwaka wa kumi na tano. Tukiwa tumekaa, mumewe alirudi toka kazini akiwa na kifuko mkononi wakati huo mazungumzo yalikuwa yamepamba moto.


Ajabu ya Mungu hakunyanyuka wala nini, alimuangalia akipita na kwenda chumbani,  aliendelea na gumzo kama hajamuona mumewe. Baada ya muda mumewe alitoka na ndoo kuelekea bafuni yeye ametulia, sikutaka kuuliza nilitaka nione mwisho wake.


Baada ya kuoga yule mwanamume alitoka kabadili nguo na kumwambia mkewe.
“Pesa za kula zipo juu ya meza na za kuwanunulia watoto madaftari.”
“Haya,” alijibu kwa mkato bila kushughulisha naye.


Baada ya mumewe kutoka ilibidi nimweke chini yule binti kutokana na kumnadi mumewe kwa vipanga wa waume za watu. Tabia zile ndizo zilizopo katika majumba yetu bila kujua tunavunja nyumba zetu kwa mikono yetu wenyewe kwa kuishi mapenzi ya mazoea.


Tukio lile lilinifanya nikumbuke enzi zangu pale nilipokuwa nikiwapata waume za watu ambao kila nilichowafanyia walichanganyikiwa, si unajua mtoto nilifundwa nikafundika kwa kujua mwanaume anataka nini. Kila niliyekutana naye alitangaza ndoa kutokana na jinsi wanavyoboreka ndani ya nyumba zao.


Shoga nyumba yako ni wewe mwenyewe unaweza kuijenga  au kuibomoa,  acha kuishi maisha ya mazoea kwa vile umeolewa  na kubakia na usemi wa “nyie wote matawi shina ni mimi.”


Huna habari shina lilitengenezwa mkaa na matawi yakachongwa kinyago kilichofika Ulaya kingine kikakaa ndani. Wewe unabakia maisha ya jalalani ukiisha kuwa majivu nani atakukumbuka. Shoga lazima uelewe kazini au katika mihangaiko kuna shuruba nyingi, mwenzako akirudi mpokee alichoshika hata kama hana, nyanyuka mpokee na kwenda naye ndani kisha mpe pole na mihangaiko.


Kama mwenye uchovu basi mkandekande baba chanja ili aone umuhimu wa kurudi nyumbani.


Mpatie maji au kahawa kisha nendeni mkaoge pamoja, umbile lako kwake dawa kwani akiliona wakati wa kuoga uchovu na mawazo yote humtoka. Ukitaka cha usiku mpe hakuna raha ya mapenzi kama kumkata kiu mpenzi popote penye nafasi. Siyo wajinga waliosema kula nanasi kwahitaji nafasi.


Mkirudi ndani shoga kaa na mumeo, ikiwezekana katika mikao ya mitego, mfanye mumeo asijute kukuoa na kujivunia kuwa nawe. Jamani siyo unasafiri mumeo anafurahi tena moyoni anasema usirudi, nataka ukisafiri hata wiki humalizi mumeo akutumie nauli.


Jamani tuache kuishi kwa mazoea na kuwageuza waume zetu kama kaka zetu, tutageuzwa walinzi wa nyumba, nyumba ndogo ndizo zionekane kubwa. Namalizia kwa kusema mazoea yako ya kupuuza baadhi ya vitu ndivyo vinatoa nafasi kwa wake wadogo.


Hakikisha kilichomvuta mumeo kwako au kilichomfanya siku za nyuma awahi nyumbani ndicho unakizidisha. Mtie hamu kwa mitego akuone mtamu, yangu ni hayo chukua udumu au yaache uachike.

No comments:

Post a Comment