POLISI saba kutoka wilayani Kasulu, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, iliyoanza kikao chake mjini Kigoma leo na kusomewa mashitaka ya kuua kwa kukusudia.
Mbele ya Jaji Sam Rumanyika, askari Polisi hao walidaiwa kuwa Agosti 6, 2011 walimpiga na kumuua kwa makusudi Festo Stephano, mkulima na mkazi wa Kijiji cha Rungwe mpya wilayani Kasulu mkoani Kigoma.
Waliopandishwa kizimbani na kusomewa mashitaka yao ni pamoja na Baraka Hongdi, Koplo Mawazo, Koplo Swahib, Koplo Charles, Koplo Shamsi, Koplo Jerry na Koplo Amrani ambao kwa pamoja walikana mashitaka.
Baada ya kukana mashitaka, kesi hiyo ilianza kusikilizwa kwa mashahidi wa upande wa Jamhuri kuanza kutoa ushahidi wao, ambapo shahidi wa kwanza katika kesi hiyo, Masumbuko Stephano, aliieleza Mahakama kwamba askari hao walikusudia kufanya mauaji hayo.
Masumbuko aliieleza Mahakama kwamba siku ya tukio, alikamatwa pamoja na marehemu na mgambo wa kijiji, na kuwekwa katika mahabusu ndogo katika Ofisi ya Mtendaji wa Kata.
Alidai baada ya kufika, askari hao walianza kuwapiga kwa kutumia vitako vya bunduki, fimbo na chupa za bia, hali iliyosababisha wapatwe na maumivu makali.
Shahidi huyo alidai kuwa baada ya kupigwa na kukaribia kupoteza fahamu, polisi hao waliwavua nguo, wakawafunika na turubai ndani ya gari ambapo baadaye walinunua magunia ya mkaa na kuwakandamiza na magunia hayo.
Shahidi wa pili katika kesi hiyo, Andrea Sama, alidai kwamba askari hao walikusudia kufanya mauaji siku hiyo, kwani licha ya kutoa kipigo pia waliwavua nguo na kuwaingiza miti kwenye sehemu zao za haja kubwa.
“Mheshimiwa Jaji kwa kweli nilishuhudia vitendo vya askari hao kwa macho yangu, na nilishindwa kuamini kama jambo hilo linafanyika kwenye ardhi ya Tanzania au tuko nchi nyingine, maana unyama uliofanywa na askari polisi hao huwezi kudhani kama ni walinzi wa amani katika nchi hii,” alidai Sama.
Kesi hiyo itaendelea kusikilizwa mfululizo hadi kutolewa hukumu, ambapo mwanasheria mwandamizi wa Serikali, Juvelin Rugaihuruza, alidai kuwa upande wa Jamhuri ambao ndiyo mlalamikaji, unatarajia kuwa na mashahidi 12 na vielelezo viwili.
Washitakiwa hao wanatetewa na Mwanasheria, Method Kabuguzi, kutoka Kampuni ya Uwakili ya Kigoma Law Chamber and Advocate ya mjini Kigoma.
No comments:
Post a Comment