Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema Lwakatare akionyesha ishara ya vidole kwa wafuasi wake katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
WAFUASI wa Chama Cha Maendeleo na Demokrasia (Chadema) jana walishindwa kuhudhuria kesi katika Chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kusikiliza kesi inayomkabili Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama Wilfred Lwakatare baada ya Mahakama hiyo kusikiliza kesi hiyo kwa usiri zaidi.
Wafuasi hao wa Chadema walifurika katika ukumbi wa Mahakama namba mbili wakisubiria kesi hiyo, lakini wakati wakisubiria katika ukumbi huo, kesi hiyo ilikuwa ikiendelea katika ‘chamber’ ya Hakimu Fimbo hadi ilipomalizika ndipo wakaarifiwa kuwa kesi imeshaisha.
Lwakatare na Rwezaura walikuwa wakikabiliwa na mashtaka manne, matatu kati yake yakiwa ya ugaidi na moja la kawaida la jinai. Mashtaka hayo yalikuwa ni kula njama, kupanga kumteka Dennis Msacky na kisha kumdhuru kwa kutumia sumu, na kufanya mkutano wa kuchochea vitendo vya kigaidi.
Mashtaka hayo matatu yalikuwa yakiwakabili washtakiwa wote wawili wakati shitaka la nne la kuhamasisha vitendo vya ugaidi lilikuwa likimkabili Lwakatare peke yake, akidaiwa kuruhusu nyumba yake ya Kimara King’ongo kutumika kupanga mipango yaugaidi.
Hata hivyo Mei 8, mwaka huu, Mahakama Kuu iliwafutia mashtaka hayo matatu ya ugaidi na kubakiwa na shtaka moja tu la kula njama za kutenda kosa la kumdhuru Msacky kwa kutumia sumu. Jitihada za mawakili wa Lwakatare, kumchomoa mahabusu jana ziligonga mwamba na sasa atalazimika kuendelea kusota mahabusu hadi Mei 27. Mawakili hao wa Lwakatare jana waliiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu impatie dhamana, baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kumfutia, mashta ya ugaidi yaliyokuwa yakimkabili yeye na mwenzake Joseph Ludovick Rwezaura, ambayo hayana dhamana.
Juzi mmoja wa mawakili hao, Peter Kibatala aliliambia Mwananchi kuwa walikuwa wamejiandaa kikamilifu kuhakikisha kuwa jana wangeweza kumtoa kwa dhamana kwa kuwa walikuwa tayari kukamilisha masharti ya dhamana kama kusingekuwa na pingamizi la kisheria kutoka upande wa mashtaka. Hata hivyo jitihada zao ziligonga mwamba jana kutokana na hakimu anayesikiliza kesi hiyo, Aloyce Katemana kutokuwepo na hivyo kesi hiyo iliahirishwa na Hakimu Sundi Fimbo hadi Mei 27.
No comments:
Post a Comment