Hivi karibuni wabunge wa Kambi ya Upinzani wameitaka Serikali kulivunja Jeshi la Polisi Tanzania na kulifanya kuwa kitengo ndani ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), kwa kile walichodai kuwa limeoza na limekithiri vitendo vya dhuluma na rushwa.
Vilevile wapinzani hao wamemtaka Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi pamoja na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Said Mwema wajiuzulu na endapo wakishindwa kufanya hivyo basi Serikali iwafukuze mara moja.
Akisoma hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi kwa Mwaka wa Fedha wa 2013/14, Dk Nchimbi amesema polisi wamekuwa na mikakati ya kupunguza uhalifu ambayo imesaidia kubaini, kuzuia na kudhibiti uhalifu na wahalifu kwa kiwango cha juu.
Amesema Serikali inajivunia jeshi hilo kwa sababu limefanya kazi kubwa kukabili kasi ya kutokea kwa vitendo vya uhalifu licha ya kuwepo kwa changamoto za uadilifu kwa askari hao, lakini wadau wa jeshi hilo hawakubaliani naye.
Ukatili wa vyombo vya dola kwa raia
Suala hilo pia limejadiliwa na wadau wa habari nchini chini ya Baraza la Habari nchini (MCT) hivi karibuni jijini Dar es Salaam, wakisema kuna ongezeko la vitendo vya ukatili wa vyombo vya dola dhidi ya raia na utamaduni wa kutowajibika nchini.
Mwanahabari mkongwe nchini, Jenerali Ulimwengu anasema kumekuwa na ongezeko la vitendo vya ukatili vinafanywa na vyombo vya ulinzi na usalama dhidi ya raia mara nyingi bila ya kuwepo sababu za maana.
Anaongeza kuwa vitendo hivyo vimekuwa ni mwendelezo wa mapokeo yanayotokana na historia ya ukoloni, na hayao yameendelea katika awamu zote hadi leo.
Akizungumzia unyanyasaji unaofanywa na vyombo vya dola, Ulimwengu analitaja Jeshi la Polisi kama mhusika mkuu, hasa kwa kuwa lilirithi silka za kikoloni na halikuundwa upya hata baada ya uhuru.
“Utawala wa awamu ya kwanza kutoka 1961 hadi 1985 uliongozwa na Mwalimu Julius Nyerere ambaye alirithi mikoba ya wakoloni vikiwamo vyombo vya ulinzi na usalama, yaani Jeshi la Polisi, Jeshi la Ulinzi na asasi maalumu yaani idara ya usalama,” anasema Ulimwengu.
Anaongeza kuwa, mwaka 1964 vikosi vya Jeshi la ulinzi (Tanganyika Riffles) lililotokana na jeshi la mkoloni la ‘Kings Africans Riffles’ liliasi na kuitikisa Serikali ya Mwalimu Nyerere ambaye baada ya kusaidiwa na vikosi vya nje, alilivunja na kuunda Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.
No comments:
Post a Comment