Tuesday, 6 August 2013

35 wauawa na wapiganaji Nigeria

Takriban watu 35 wameuawa katika mashambulizi matatu yaliyofanywa na wapiganaji wa kiisilamu nchini Nigeria, kwa mujibu wa maafisa wakuu wa serikali.
Taarifa kutoka kwa jeshi, zinasema kuwa wapiganaji 32, wanajeshi wawili na polisi walifariki kwenye mashambulizi hayo, yaliyofanywa dhidi ya kituo cha polisi na dhidi ya kambi ya jeshi siku ya Jumapili.
Sheria ya hali ya hatari imewekwa katika jimbo la Borno na majimbo mengine mawili mnamo mwezi Mei baada ya miaka minne ya mashambulizi yanayofanywa na kundi la wapiganaji la Boko Haram.
Kundi hilo lilianza harakati zake mwaka 2009 za kutaka kuligeuza eneo zima la Kaskazini mwa Nigeria kuwa chini ya sheria za kiisilamu.
Zaidi ya watu 2,000 wameuawa tangu kundi hilo kuanza harakati zake.
Mashambulizi hayo mawili katika jimbo la Borno yalifanyika siku ya Jumapili, lakini taarifa za mashambulizi hayo ndizo zimejitokeza tu.
Mawasiliano katika eneo hilo yametatizika tangu sheria ya hali ya hatari kutangazwa .
'Wanajeshi hata hivyo walifanikiwa kuwafurusha wapiganaji wa kiisilamu wa Boko Haram, walionuia kufanya mashambulizi dhidi ya kambi ya jeshi eneo la Bama... Tarehe 4 mwezi Agosti.
Jeshi pia lilisema kuwa kambi ya jeshi mjini Malam Fatori lilishambuliwa na hivyo kusababisha ufyatulianaji wa risasi.
Hata hivyo Boko Haram haijatoa tamko lolote kuhusu mashambulizi hayo.
 
Harakati za jeshi dhidi ya Boko Haram

No comments:

Post a Comment