Askari wa Kenya wakiwa juu ya jengo la Westgate jana kuwasaka magaidi walioteka watu tangu Jumamosi.
Nairobi. Wakati jengo la ghorofa tatu
lililovamiwa na magaidi likiripotiwa kuanguka jana na kuua watu sita,
Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta amesema mwanamke mmoja raia wa Uingereza
na Wamarekani wawili au watatu wanashukiwa kuongoza shambulizi la
kigaidi lililofanywa katika jengo la biashara eneo la Westgate, Nairobi,
Jumamosi iliyopita.
Akilihutubia taifa la Kenya jana, Rais Kenyatta
alisema hakuna ushahidi wa kuwahusisha watu hao na tukio hilo moja kwa
moja lakini uchunguzi unaendelea.
“Wataalamu wa mambo ya upelelezi wanaendelea
kuchunguza juu ya ushiriki wa watu hawa na wakiwabaini, basi tutachukua
hatua kali,” alisema Rais Kenyatta.
Tangu kutokea kwa shambulizi hilo, vyombo
mbalimbali vya habari vilimtaja mwanamke wa Uingereza, Samantha
Lewthwaite kuwa ndiye aliyeongoza shambulizi hilo.
Pia jina lake lilitajwa na Kundi la Al-Shabaab kupitia katika mtandao wa mawasiliano wa kijamii wa Twitter.
Hata hivyo, maelezo ya Rais Kenyatta yanapingana
na ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi hiyo, Joseph ole Lenku ambaye
alikaririwa na vyombo vya habari jana akidai kuwa hakukuwa na mwanamke
miongoni mwa magaidi hao, bali baadhi yao walivaa nguo za kike.
Rais Kenyatta alisema magaidi watano walikuwa wameuawa katika operesheni hiyo ya kulikomboa jengo hilo.
Pia alibainisha kuwa watu kumi na moja walikuwa wanashikiliwa na polisi wakishukiwa kushiriki katika shambulio hilo.
Magaidi wanaoaminika kuwa wafuasi wa Kundi la
Al-Shabaab walivamia jengo hilo na kufanya shambulizi lililosababisha
vifo vya zaidi ya watu 60 na 175 kujeruhiwa, Jumamosi iliyopita.
Rais Kenyatta aliapa kuwa Serikali yake imepania kuwashinda magaidi na kuhakikisha inawafikisha kwenye mikono ya sheria.
Ghorofa kuanguka
Pia Rais Kenyatta alitangaza kuwa maofisa sita wa
usalama walifariki dunia jana jioni baada ya kuangukiwa na ukuta baada
Alisema watu hao walifukiwa na ukuta wakati vikosi vya usalama vikiendelea na operesheni ya kuwasambaratisha magaidi hao.
Rais Kenyatta alieleza kuwa haijajulikana mara moja chanzo cha kuanguka kwa ukuta huo na kwamba wanachunguza jambo hilo.
Hali hiyo inafanya idadi ya watu waliokufa kufikia
67. Kati yao, 61 wakiwa ni watu wa kawaida na sita ni maofisa wa
usalama, huku 175 wakiwa wamejeruhiwa.
Siku tatu za maombolezo
Rais Kenyatta alitangaza siku tatu kwa ajili ya maombolezo kutokana na shambulizi hilo la magaidi.
Alisema bendera za Kenya zitapepea nusu mlingoti kuanzia leo ili kuwakumbuka watu waliopoteza maisha katika tukio hilo.
“Maombolezo haya ni kwa ajili ya kuwakumbuka
wenzetu waliopoteza maisha kutokana na kitendo hiki cha kikatili cha
watu waoga,” alisema Rais Kenyatta.
Amshukuru Rais Kikwete
Pamoja na kuwashukuru wananchi wa Kenya, pia Rais
Kenyatta alimshukuru Rais Jakaya Kikwete na viongozi wengine wa Afrika
Mashariki kwa kuwafariji katika kipindi hiki kigumu.
“Ninaomba kuwashukuru Marais Yoweri Museveni wa
Uganda, Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania, Paul Kagame wa Rwanda, Salva
Kiir wa Sudan Kusini na Pierre Nkuruzinza wa Burundi kwa kutuunga mkono
katika kipindi hiki kigumu,” alisema Rais Kenyatta na kuongeza:
“Viongozi hawa wamekuwa wakiwasiliana nami kila wakati kujua tunavyoendelea na operesheni.”
Pia Rais Kenyatta aliwashukuru wananchi wa Kenya kwa kuwa kitu kimoja katika kipindi hiki na kujitolea kwao kwa hali na mali.
ya kudondoka kwa ghorofa tatu za jengo ambalo magaidi wamejichimbia.
No comments:
Post a Comment