UAMUZI wa kuingia kwenye uhusiano wa kimapenzi si sawa na
kufanya uchaguzi wa aina ya chakula unachopenda kula. Haufanani na uamuzi wa kuchagua
muda wa kulala. Haufanani na kitu chochote kile.
Ni uamuzi makini, ambao unahitaji utulivu na uamuzi wa ndani. Si
kukurupuka, maana mwisho wake unaweza kuwa machozi. Hebu jiulize, wewe ambaye
unataka kuanzisha uhusiano wa kimapenzi upo tayari?
Suala la utayari
halikuhusu wewe kama wewe kwa uamuzi binafsi na hisia zako za ndani pekee,
lazima uwe na sifa muhimu ambazo zinakidhi wewe kuwa na mwenzi. Tupo pamoja
marafiki?
Yapo mambo ya msingi
ambayo lazima yawe yametimia kwako, ndipo uwe na hadhi ya kuwa mpenzi wa mtu.
Wanasaikolojia ya Uhusiano, wameelekeza wazi vipengele muhimu ambavyo kijana
anapaswa kuvizingatia kabla hajaamua kuingia katika uhusiano wa kimapenzi.
Hata hivyo, tafiti
mbalimbali zinaonesha kuwa vijana wengi wanaobalehe au kuelekea kubalehe huwa
hawafahamu vipengele hivyo muhimu na hata hao wachache waliopata elimu hiyo
elekezi bado hujikuta wakishindwa kufuata taratibu hizo kulingana na mazingira.
Vipo vitu vingi vya kuzingatia,
lakini nitafafanua vile vya msingi zaidi, ambavyo vitakuongoza wewe kijana
kabla ya kuamua kuingia kwenye uhusiano.
Ni mada nzuri zaidi kwa
vijana ambao bado hawajaanza uhusiano, lakini hata kwa aliyeanza, itamsaidia
kujua yupo katika kundi gani na nini cha kufanya. Lazima kuna kitu cha
kujifunza katika mada hii. Twende darasani.
SUALA LA UMRI
Hili ni la kwanza kati ya yale muhimu zaidi ya kuzingatiwa,
lazima uangalie una umri gani? Inawezekana ukawa na umri ambao unadhani una
uwezo mkubwa wa kupanga na kuamua mambo yako lakini kumbe siyo!
Unaweza ukaingia katika uhusiano, ukadumu humo kwa muda mrefu
sana, lakini wakati huo ukiendelea kukua kiakili, hapo sasa ndipo utakapogundua
kuwa kuna makosa uliyofanya awali.
Inashauriwa kwamba vijana ambao wana umri chini ya miaka 18,
wasijiingize kabisa katika uhusiano. Huu ni ushauri na mahali pengine siyo
ushauri ni lazima! Kama unajijua upo chini ya umri huu, achana kabisa na
mapenzi, huu ni muda wako wa kupanga maisha yako ya baadaye.
KWA WANAFUNZI...
Inawezekana ukawa na umri zaidi ya miaka 18, lakini ukawa
masomoni, je unaruhusiwa kuwa na mpenzi? Jibu ni hapana...wewe uliye masomoni
hususan Elimu ya Msingi na Sekondari hushauriwi kuwa katika uhusiano kwa
kipindi hiki. Masomo ni magumu sana kwa ‘levo’ hii na inawezekana ukashindwa
kufanya mitihani yako vizuri kutokana na kuwaza mambo mawili kwa wakati mmoja.
Kimsingi ni vitu viwili tofauti ambavyo havichanganyiki. Hii
siyo amri, ni ushauri tu! Kama kweli unataka kufanikiwa katika maisha yako ya
baadaye, soma kwanza
achana na mambo ya mapenzi katika kipindi hiki.
Andaa maisha yako kwanza. Siku moja ukiwa mitaani baada ya
kumaliza masomo, ikiwa utabahatika kusoma makala haya kwa mara nyingine
gazetini, mtandaoni au hata kwenye kitabu, utajuta na inawezekana ukalia,
wakati huo muda utakuwa umeshapita!
FEDHA INAHUSIKA?
Mapenzi na fedha ni vitu viwili tofauti rafiki zangu, lakini
kuna wakati fedha inakuwa na nafasi yake katika mapenzi. Siyo kwa maana ya
kuhonga au kununua penzi, lakini kwa ajili ya mahitaji ya hapa na pale.
Sasa jiulize, ikiwa wewe ni mwanafunzi, unayetegemea kupewa
fedha za matumizi na wazazi wako, utawezaje kugharamia penzi lako?
Ikiwa umekwishamaliza masomo yako, na umri wako unaruhusu (zaidi
ya 18), kipengele hiki hakikuhusu, maana penzi la dhati halizingatii fedha.
Kama upo masomoni, basi yakupasa usome kwa bidii hadi utakapomaliza masomo
yako, mapenzi yapo, utayakuta!
IPO DAWA!
Najua wengi watakuwa na maswali mengi, kwamba kwa sababu tu, mtu
anasoma ndiyo asiwe na mpenzi? Au mwingine anawaza atawezeje kuishi bila kuwa
na kampani ya jinsia tofauti? Hayo yote ni mawazo yenye maana kubwa katika mada
hii. Wataalam wanawashauri wanafunzi kuwa mbali na mapenzi, kwa sababu mapenzi
huteka hisia, muda mwingi huweza kuutumia kumuwaza mpenzi zaidi kuliko masomo,
sasa kuna haja gani ya kuchanganya mambo wakati inawezekana kuacha?
Haikatazwi kuwa na rafiki wa jinsi tofauti na yako, lakini iwe
kwa wema. Kuna mambo mengi unaweza kufanya na rafiki yako kuliko kuwa katika
uhusiano wa kingono. Itapendeza kama mtasaidiana kimasomo au kuanzisha mijadala
itakayowapa mwanga wa maisha yenu yajayo.
Pamoja na hayo, najua ni vigumu sana kuweza kudhibiti hisia,
lakini hilo linawezekana kama utakuwa mtu wa mazoezi, msomaji wa vitabu
mbalimbali vitakavyokujenga na mengineyo.
Mchukie kama rafiki yako wa kawaida, weka hisia za mapenzi
pembeni, endelea na maisha yako na siku moja muda ukifika na ukiwa tayari
utaingia katika uhusiano makini utakaokufurahisha siku zote za maisha yako.
MUHIMU
Katika vipengele vyote nilivyoanisha hapo juu, hasa katika
kijisehemu cha kipato na masomo, haviwahusu wanafunzi wa vyuo! Hii inakuwaje?
Kwa sababu wengi wao huwa ni watu wazima tayari, wenye ufahamu juu ya mambo
mbalimbali ya maisha yao. Wanajua kupambanua mambo na wanajua wanachokifanya.
Wengine huwa tayari wapo katika ndoa au kuingia katika ndoa
wakiwa vyuoni, hawa vipengele hivyo haviwahusu. Pamoja na hayo, angalia moyo
wako unazungumza nini kabla ya kuingia katika uhusiano. Naamini nimeeleweka.
Tukutane hapa wiki ijayo kwa mada nyingine kali.
No comments:
Post a Comment