Dar es Salaam.Rais Mstaafu,
Benjamin Mkapa jana aliadhimisha miaka 75 ya kuzaliwa kwake kwa kufanya
Ibada ya Misa iliyoongozwa na Askofu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam,
Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo.
Katika ibada hiyo ya shukrani iliyofanyika Kanisa
Katoliki la Maria Imakulata, Upanga jijini Dar es Salaam, Mkapa
aliwataka Watanzania kumshukuru Mungu kwa kila jambo.
“Tunamshukuru Mungu kwa majaliwa aliyoipatia nchi
yetu ya Tanzania na tunamwomba azidi kuijalia umoja katika yote
tunayofanya na tunayokusudia kuyafanya,” alisema Mkapa.
Mkapa pia aliwashukuru waumini wenzake katika
kanisa hilo, huku akifichua siri kwamba, Kadinali Pengo alimtaka ahamie
Kanisa la Mtakatifu Joseph wakati alipokuwa rais, lakini hakukubali.
Kwa upande wake, Kardinali Pengo aliwataka Watanzania kuwa na tabia ya kumshukuru Mungu kwa kila jambo.
“Alichofanya Rais Mstaafu Mkapa ni cha kuigwa.
Tunatakiwa kutambua kuwa hatuishi kwa nguvu zetu bali kwa uwezo wa Mungu
hivyo ni lazima tumshukuru kama alivyofanya mwenzetu,” alisema
Kardinali Pengo.
Baadhi ya viongozi waliohudhuria ibada hiyo ni
pamoja na Mawaziri Wakuu Wastaafu, Edward Lowassa na Cleopa Msuya,
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu wa Bunge), William
Lukuvi na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia.
Wengine ni waziri wa zamani, Profesa Philemon
Sarungi, Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT),
Dk Alex Malasusa pamoja wakuu wa zamani wa Jeshi la Wananchi wa
Tanzania (JWTZ), Majenerali, Robert Mboma na George Waitara.
No comments:
Post a Comment