Familia inayowajumuisha baba, mama na mtoto ni miongoni mwa abiria 25 walipoteza maisha katika ajali za barabarani zilizotokea katika mikoa ya Singida, Lindi na Kilimanjaro.
Omari Shaban (44), mke wake Salma Omari na mtoto
wao Nyamumwi Omari (10) wakazi wa Itigi, Singida, walifariki dunia baada
ya gari walilokuwa wakisafiria aina ya Noah kugongwa na lori aina ya
Scania katika ajali iliyosababisha vifo vya watu 13 mkoani humo.
Ajali hiyo ilitokea saa 1:32 asubuhi katika Kijiji
cha Isuna, Wilaya ya Ikungi, Barabara Kuu ya Singida-Dodoma, ambapo
watu watatu walinusurika na kupata majeraha madogo madogo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Singida, Geofrey
Kamwela alisema Noah lilikuwa likitoka Itigi, wilayani Manyoni kwenda
Singida Mjini na kwamba miili ya watu 10 walikuwa wameshatambuliwa na
ndugu zao hadi jana mchana.
Alisema magari hayo yalikuwa yakipishana, lakini
ghafla lori lilihama upande wake na kulifuata Noah upande wa kushoto mwa
barabara, ambako lililigonga, kisha kuliburuza.
“Kwa sasa bado hatujajua chanzo cha ajali hiyo
mbaya ingawa baadhi ya watu wanadai kuwa huenda dereva wa lori alisinzia
na kusababisha lori hilo kuhama upande wake na kulifuata Noah. Uchuguzi
utakapokamilika, tutatoa taarifa,” alisema Kamwela.
Aliwataja wengine waliofariki katika ajali hiyo
kuwa ni Mkazi wa Msisi, Haji Mohammed (29), Wakazi wa Sajaranda; Mtunku
Rashidi (68), Salehe Hamisi (28), Athumani Kalemba (38) na Ramadhan
Mkenga, Mkazi wa Puma, Samir Shaban (20) na Mwaleki Nkuwi (35) ambaye ni
mkazi wa Ikungi.
Miili ya abiria hao pamoja na watatu ambao
walikuwa hawajatambuliwa, imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia
maiti cha Hospitali ya Mkoa wa Singida.
Mganga mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk Banuba Deogratius amekiri kupokea miili ya watu 13 na kwamba kati yao, watoto ni wawili.
JK atuma salamu
Rais Jakaya Kikwete ametuma salamu za pole kwa
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Perseko Kone kutokana na vifo vilivyotokea
katika ajali hiyo.
“Nimeshtushwa, nimesikitishwa na kuhuzunishwa mno
na taarifa za vifo vya watu 13 akiwemo mtoto wa miezi minne,” alisema
Rais Kikwete katika taarifa iliyotolewa na Ikulu jana.
Rais alisema inasikitisha pale makosa ya kibinadamu katika
uendeshaji wa vyombo vya moto yanapoendelea kusababisha ajali ambazo
zimekuwa chanzo cha kupoteza maisha ya watu wasio na hatia wakiwamo
watoto, kusababisha ulemavu wa kudumu na uharibifu wa mali.
“Kupitia kwako (mkuu wa mkoa), naomba unifikishie
salamu zangu za rambirambi na pole nyingi kwa familia zote zilizopoteza
wapendwa wao katika ajali hiyo. Nawaomba wanafamilia wawe na moyo wa
uvumilivu, subira na ujasiri hivi sasa wanapougulia machungu ya
kupotelewa na ndugu zao,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.
No comments:
Post a Comment