Monday, 20 January 2014

Wapinga Kawambwa kubakizwa elimu

Wizara ya Elimu imekuwa na matatizo kwa muda mrefu, ingawa watu wanasema wakati wa Dk Kawambwa hali imekuwa mbaya zaidi, sioni kama Jenista atakuja na miujiza,”


Baadhi ya wadau wa elimu wamesema kubakizwa kwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa na kumwondoa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo hakuwezi kuleta mabadiliko yoyote kwani Waziri ndiye msimamizi mkuu wa sera.

Wakitoa maoni yao jana kuhusu mabadiliko kwenye wizara hiyo, baadhi yao walisema hakutakuwa na miujiza kutoka kwa Jenista Mhagama aliyeteuliwa kuwa Naibu Waziri, kwani moja ya matatizo makubwa ya wizara ya elimu ni mfumo. Profesa Justinian Galabawa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema 

kinachotakiwa ili kuinua sekta ya elimu ni kubadili mfumo wa elimu kuanzia shule za msingi mpaka sekondari.
Alisema kazi kubwa inatakiwa kufanywa na watalaamu na wahakikishe wanasimamia kazi zao ikiwa ni pamoja na vifaa vya kujifunzia kama vitabu, upatikanaji wa walimu wenye sifa na wanaoweza kutekeleza majukumu yao.
Alisema kuwa kwa kufanya hivyo sekta ya elimu itapata mabadiliko na siyo kupunguza alama za ufaulu kama wanavyofanya sasa.
“Nashindwa kuelewa kwa nini wanapunguza alama za ufaulu na hivi juzi tena nimeona wamepunguza za kidato cha pili,” alisema Profesa Galabawa. Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la HakiElimu, Elizabeth Missokia, alisema haoni kama kuna mabadiliko ndani ya wizara hiyo kwani waziri aliyekuwa akilalamikiwa ndiye huyohuyo aliyebaki.
“Kumwondoa (Philipo) Mulugo haitoshi, Jenista Mhagama sijawahi kumwona akiwa waziri kwenye wizara yoyote, namwona tu akiongoza vikao vya Bunge, yeye kuwa mwalimu haiwezi kusaidia kwa sababu hata Mulugo alikuwa mwalimu.
“Wizara ya Elimu imekuwa na matatizo kwa muda mrefu, ingawa watu wanasema wakati wa Dk Kawambwa hali imekuwa mbaya zaidi, sioni kama Jenista atakuja na miujiza,” alisema Misokia.
Alisema kwamba ni vizuri Mhagama akajua kuwa, anaenda kwenye wizara iliyo na changamoto nyingi hivyo kusimamia upatikanaji wa sera bora, kukabili kero za walimu, akijituma atafanikiwa.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Kitila Mkumbo, alisema kuwa haoni kama kuna mabadiliko kwani waziri ambaye ndiye msimamizi mkuu wa sera bado yupo yuleyule.

No comments:

Post a Comment