Rais Kikwete alikutana na Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal Ikulu kujadili uteuzi huo.
Ripoti ya Kamati Ndogo ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira iliyoundwa kuchunguza Operesheni Tokomeza ndiyo iliwang’oa mawaziri hao baada ya kueleza athari zilisababishwa na wizara nne walizokuwa wakiziongoza.
Wakati Watanzania wakisubiri kwa hamu mabadiliko ya Baraza la Mawaziri, Rais Jakaya Kikwete amekuwa akikuna kichwa kupanga safu yake huku Ikulu ikiwataka wananchi kuwa watulivu katika kipindi hiki.
Tangu mawaziri wanne, Dk Emmanuel Nchimbi (Mambo
ya Ndani), Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na JKT), Balozi Khamis Kagasheki
(Maliasili na Utalii) na Dk David Mathayo (Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi)
walipovuliwa nyadhifa zao ikiwa ni hatua ya kuwajibika kutokana na
madhila yaliyowapata wananchi kutokana na Operesheni Tokomeza Ujangili,
na kifo cha aliyekuwa Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa, kumekuwa kuna
kila aina ya uvumi.
Hata hivyo, kitendawili kilichobakia ni siku gani
hasa Rais Kikwete atakapotangaza mawaziri wapya kwani hata wasaidizi
wake wamekuwa wakikwepa kuzungumzia suala hilo na kuwataka wananchi
kuvuta subira.
Taarifa zilizofikia gazeti hili jana, zilieleza
kuwa Rais Kikwete alikutana na Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal
Ikulu kujadili uteuzi huo.
Utaratibu unaelekeza pale Rais anapofanya uteuzi wa mawaziri hushauriana na Makamu wake na Waziri Mkuu.
Chanzo kimoja kilidokeza kuwa kikao baina ya viongozi hao wawili kitaifa kilianza jana mchana.
“Kaka nakueleza tu wakuu wamekutana na hivi sasa
ninavyoongea na wewe wanaendelea kujadili suala hilo ila sina uhakika
mabadiliko haya yatangazwa lini,” kilidokeza chanzo hicho.
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Katibu Mkuu
Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alisema: “Wananchi watulie na kumpa nafasi
Rais Kikwete kupanga safu yake ya mawaziri. Siwezi kusema atatangaza
lini kwa sababu siwezi kumpangia siku ya kutangaza baraza, nadhani
tusibiri tu mpaka siku atakapotangaza ndipo tutajua.”
Aliongeza: “Najua watu wana shauku kubwa lakini wanatakiwa kutulia tu muda mwafaka ukifika, kila kitu kitawekwa wazi.”
Balozi Sefue alisema uteuzi huo ni mzito na
unahitaji umakini na muda huku akigoma kutoa ufafanuzi baada ya kuulizwa
kuhusu kufanyika kwa kikao kati ya Rais na Makamu wake.
Uteuzi huo unafanyika baada ya Desemba 20 mwaka
jana Rais Kikwete kutengua uteuzi wa mawaziri hao kutokana uchunguzi
uliofanywa na kamati ndogo ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira
iliyoongozwa na James Lembeli.
Ripoti ya Kamati Ndogo ya Bunge ya Ardhi,
Maliasili na Mazingira iliyoundwa kuchunguza Operesheni Tokomeza ndiyo
iliwang’oa mawaziri hao baada ya kueleza athari zilisababishwa na wizara
nne walizokuwa wakiziongoza.
No comments:
Post a Comment