Polisi wilayani Kaliua, inadaiwa kumuua mtu mmoja na kumjeruhi mwingine baada ya wananchi zaidi ya 200 kuvamia kituo kidogo cha polisi kwa lengo la kumtoa mtuhumiwa ili wajichukulie sheria mkononi.
Tukio hilo limetokea baada ya wananchi wa Kijiji
cha King’wangoko, Kata ya Sasu kuvamia kutaka kumdhuru Shija Matenga,
anayetuhumiwa kuiba ng’ombe watano Kasulu, Kigoma.
Kamanda wa Polisi mkoani Tabora, Kamishna Msaidizi
wa Polisi, Peter Ouma, akielezea tukio hilo alisema Mkuu wa Kituo
Kidogo cha King’wangoko, Sajenti Kimola alipokea simu kutoka kwa Wakala
wa Mnada wa Konanne, kuwa wananchi wamemkamata na wanataka kumuua.
Kutokana na hali hiyo, Sajenti Kimola alituma
askari wawili wakiwa na silaha na kumwokoa mtuhumiwa na kuanza kuondoka
naye kitendo kilichokasirikiwa na wananchi walioanza kurusha mawe na
fimbo ili kuwazuia askari wasimpeleke kituoni hali hiyo ilichosababisha
askari kupiga risasi hewani kuwatawanya wananchi.
“Askari walitumwa walifanikiwa kumwokoa mtuhumiwa
jambo ambalo liliwachukiza wananchi waliotupa mawe na fimbo ili kuwazuia
askari wasiondoke na mtuhumiwa ambao walilazimika kufyatua risasi
hewani kuwatawanya,”alisema Ouma.
Kwa mujibu wa Kamanda Ouma, baada ya askari
kumfikisha mtuhumiwa kituoni na kumfungia mahabusu, wananchi
walifuatilia na kufika kituoni alipo mtuhumiwa na kushinikiza atolewe.
Alisema askari walipoona wananchi wanataka kutumia
nguvu walifyatua risasi hewani kuwatawanya na bahati mbaya risasi moja
ilimpata John Joseph bega la kulia kufariki papohapo.
Mwingine aitwaye Malembeka Matemele alijeruhiwa
kwenye paja la mguu wa kulia na amelazwa Hospitali ya Wilaya ya Urambo.
kwa matibabu.
No comments:
Post a Comment