Kama mwanaume lazima upate wakati wa kujua unatakiwa kufanya nini kwa ajili ya kulifanya penzi lako lizidi kuchanua.
USAFI BINAFSI
Asilimia
kubwa ya wanawake wanapenda sana usafi. Ni aghalabu sana kukutana na
mwanamke asiyejipenda. Ndiyo maana wanaitwa mapambo ya nyumba au la
nyumba! Ni kwa sababu ya hulka yao ya kupenda sana usafi.
Mwanamke
anavutiwa sana na mwanaume mtanashati. Usafi wako unamfanya ajiamini
kuwa na wewe. Hata nyumbani kwako, lazima uishi katika nyumba safi. Hata
anapokuja kukutembelea, anakuta mazingira masafi kuanzia sebuleni hadi
chumbani.
Anapokukuta katika hali ya usafi, inakuwa rahisi zaidi yeye kuanzia hapo alipokukuta na kuendelea mbele.
KUJIAMINI
Mwanamke
anajisikia salama zaidi akiwa na mwanaume ambaye anajiamini – mwenye
uwezo wa kutetea hoja zake na kujieleza sawia. Siyo anayebabaika. Suala
la msimamo binafsi, kwa mwanamke ni kubwa kuliko hata kumnunulia
manukato mapya!
Mathalani unakuwa naye katika mtoko, angependa
kukuona ukiwa katika hali halisi ya maisha yako, usiyeyumbishwa na
mwenye kutoa maamuzi yasiyoyumba.
Wakati mwingine, mwanamke anaweza
kukupima hata katika jambo ambalo amekosea yeye, ataangalia unavyotoa
maamuzi yako, lakini pia atafuatilia kuona kama utakuwa mwepesi wa
kuyabadilisha.
Anataka kuona msimamo wako muda wote. Mwenye kujiamini na mawazo yasiyo na matege wala makengeza!
KUJITETEA
Kipengele
hiki hakina tofauti kubwa sana na kilichopita, lakini hapa ni kwenye
upande wa kujitetea zaidi. Wakati unapodai haki yako mbele ya mwanamke
wako, suala la kujitetea linapewa nafasi kubwa sana.
Wanawake
hawapendi kuwa na wanaume ambao wapo tayari kuonewa. Wanataka wenye
uwezo wa kusimama kidete kuona haki zao hazichukuliwi kirahisi.
Hili
si suala la kutetea tu haki yako pekee kama mwanaume, bali inapobidi
kusimamia haki ya mwanamke wako. Nisieleweke vibaya katika hili, lakini
mwanaume imara ni yule ambaye ana nguvu – anafanya mazoezi na ambaye
yupo tayari kwa lolote!
Inapowezekana, uwe na uwezo wa ‘kuzichapa’
ikiwa mtakutana na vibaka au watu wabaya wenye lengo wa
kukudhuru/kuwadhuru au kumdhuru mpenzi wako.
Mwanaume aliye ‘fiti’ ni chaguo la wanawake wengi. Si mnyonge. Mpole kupitiliza na aliye tayari kuonewa! Huyu hana nafasi.
KUJALI
Wanawake
wanapenda sana wanaume wanaojali. Wanawaona wao ni kila kitu na
wanaotoa kipaumbele kwao. Kama huna tabia hiyo, ujue upo katika nafasi
kubwa ya kumkwaza mpenzi wako. Mjali mpenzi wako kwa kila hali.
Kumjulia hali kila wakati na kutaka kujua maendeleo yake, kutakupa nafasi kubwa sana ya kuendelea kudumu katika uhusiano hai.
UKARIBU
Kati
ya vitu vinavyowapa mshawasha mkubwa wanawake ni pamoja na kusogezwa
karibu. Hapa ni kuwa naye katika mambo mengi unayoyafanya kila siku.
Ni
vizuri kuwasiliana naye mchana, ukitaka kujua aina ya chakula
alichokula siku hiyo au ikiwezekana mchagulie. Ni mambo madogo sana
lakini yanayoongeza nakshi katika mapenzi.
Yapo mengi sana ambayo kwa
kuyafanya utakuwa umemsogeza mpenzi wako karibu yako. Hebu tumia
ubunifu wako ili uweze kuteka hisia za mwenzi wako kisawasawa!
KUMSIFIA
Wanaume wengi hupuuzia hili, huona kama ni jambo lisilo na maana sana
kwao na wenzi wao. Hali ni tofauti sana kwa wanawake ambao hupenda
kuwasifia wanaume zao. Nitakupa mifano miwili ya namna wanandoa wa
jinsia mbili tofauti wanavyotambulishana kwa jamaa zao.
MWANAUME:
“Peter kutana na mke wangu, anaitwa mama Diana. Nipo naye mwaka wa tatu
sasa, tuna watoto wawili, huyo Diana na mwingine anaitwa Cris. Mama
Diana, huyu ni Peter nilisoma naye A – Level, Tosamaganga Sekondari.”
MWANAMKE: “Suzan, huyu ndiye mume wangu mpenzi...anaitwa Elifaraja
lakini mimi napenda zaidi kumuita Elly. Kiukweli nampenda sana mume
wangu jamani, tuna mtoto wetu mmoja, anaitwa Agness. (Akimgeukia mumewe)
Baby, huyu hapa ni rafiki yangu Suzan. Yaani tumekua naye mtaa mmoja
huko Arusha.”
ANGALIA TOFAUTI
Bila
shaka kwa namna wawili hao walivyotambulishana unaweza kuona tofauti
kubwa. Mwanaume amemtambulisha mkewe kawaida kabisa, hajaonesha
manjonjo au namna anavyompenda na kumthamini mwenzake, lakini mwanamke
amefanya hivyo.
Sikia nikuambie, KUMSIFIA mwanamke, kuna nafasi
kubwa sana kwake. Chunguza kwa makini, hata kunapokuwa na mgongano
katika familia, halafu wakatokea wageni, baada ya utambulisho na
mazungumzo ya hapa na pale, wageni wakiondoka kunakuwa na uwezekano
mkubwa zaidi wa kumaliza mpasuko katika familia.
Jenga utamaduni wa
kumsifia mpenzi wako, unamuweka katika kilele cha upendo. Anajiona
kamili, peke yake na mwenye nguvu kwako. Anajiamini na unamfanya azidi
kukupenda kwa kuwa anaamini yupo na mwanaume ambaye anajivunia kuwa
naye.
MALENGO
Wanaume
wengi wana ulemavu mmoja; hawapendi kuwashirikisha wanawake katika
mambo yao. Wanapenda kufanya mambo yao kwa siri na wakati mwingine
ikilazimika kumwambia mkewe basi kwa mshtukizo baada ya kukamilisha
jambo husika.
Hii si sahihi. Dunia ya leo imebadilika rafiki zangu.
Inawezekana wazee wa zamani walikuwa sahihi, maana ilikuwa ni suala la
kununua ng’ombe na kuwaweka katika zizi kwenye kijiji cha jirani, halafu
wanapewa malisho mazuri, baada ya miaka miwili wanazaliana, hapo ndipo
anamweleza mkewe.
Siku hizi dunia imebadilika, kuna mambo mengi.
Kuna suala la hasara katika biashara, utapeli n.k. Mkeo ndiye rafiki
yako mkubwa kuliko wote, ndiye ndugu yako wa karibu zaidi kuliko yeyote.
Yes! Mkeo ndiye ndugu yako maana umetengeneza naye familia.
Mmeshirikiana kuzaa watoto na kujenga maisha pamoja.
Yeye anapaswa
kujua mambo yako, ndiye mtetezi wako nambari wani. Mweleze juu ya
malengo yako, wakati mwingine anaweza kukusaidia sehemu ambayo
hukutarajia.
Hata hivyo, kumshirikisha katika malengo yako, kunampa
nguvu na nafasi ya kujiona mama katika familia yenu. Msaidizi kamili wa
nyumba yenu.
KIPAUMBELE
Kuna
wakati wanawake huwa na mambo yao binafsi. Kazini au kifamilia.
Inawezekana akatatizika katika eneo fulani ambalo kwa namna moja ama
nyingine atahitaji usaidizi wako. Ikitokea mkeo akawa katika hali hiyo,
msikilize.
Mathalani ana tatizo la kifamilia, amekuambia mmoja wa
wazazi wake anaumwa, msaidie. Si lazima kifedha, lakini kuonesha kujali
kwako tu, kutampa matumani kwamba anaishi na mtu sahihi. Acha kupuuza
mambo yake; hata yale madogo, kama ya ‘mtoto wa dada amerudishwa ada
shuleni’.
Msikilize, mshauri panapofaa kufanya hivyo na ukiweza
msaidie hata kifedha. Katika upande wa pili ni hivyo hivyo. Labda una
tatizo binafsi, kazini kwako au kifamilia, mshirikishe.
Unaweza
kushangaa jambo ambalo uliamini unaweza kulimaliza peke yako, kwa
kumshirikisha likawa jepesi zaidi na mambo yakaendelea vyema.
Kipaumbele kwa namna yoyote ile, kunaongeza mapenzi zaidi kwa mwanamke.
TENDO LA NDOA
Hiki ni kipengele nyeti, kinachohitaji lugha nzuri ya kirafiki kukifafanua. Hakuna siri, tendo la ndoa ni moja ya kiwakilishi cha ndoa. Maana hata maandiko yanasema: “Mwanamke ataacha wazazi wake na kwenda kwa mumewe, nao watakuwa mwili mmoja.”
Kimsingi tendo la ndoa
lina nafasi yake. Ni muhimu likaheshimiwa na kutengewa muda maalum wa
kufurahia. Si papara. Kwa bahati mbaya wanaume huwa si wafuatiliaji
sana wa kujua namna ya kuwafurahisha zaidi wenzao. Wenyewe wanajiwazia
wenyewe. Wanafikiria namna ya kuwakomoa wenzao.
Si sahihi. Tendo la ndoa
halina maana ya kukomoana. Jenga mazoea ya kufanya maandalizi kamili
kabla ya tendo. Sikiliza hisia za mwenzako. Ukiweza kumjulia mke wako
katika eneo hili, ni wazi kwamba utazidisha upendo wake kwako, lakini
pia atakuwa katika kuta za uaminifu. Akatafute nini nje wakati wewe
ndiye mganga wake unayeweza kumtibu barabara?
Kuna kitu nimesahau
kweli? Kama kipo nitafute pembeni, kwa hapa haya yatoshe kukufanya
uelewe nilichotaka kukuelekeza. Nikuache na neno moja; uamuzi wa kuijenga ndoa yako upo mikononi mwako. Ukitaka iwe shaghalabaghala, pia ni wewe tu!
No comments:
Post a Comment