Thursday, 16 January 2014

Kaburi lafukuliwa, maiti aachwa mtupu

Shabani alisema, tukio hilo ni la kwanza kijijini hapo na kwamba kufukuliwa kwa kaburi hilo kunaonyesha kulifanywa na watu.


Wakazi wa Kijiji cha Ilagala mkoani hapa,wamepatwa na bumbuwazi baada ya kukuta kaburi limefukuliwa na maiti ikiwa tupu bila sanda.

Tukio hilo limetokea Januari 14, 2014 katika Kijiji cha Ilagala Wilaya ya Uvinza mkoani hapa ambapo wakazi hao walistaajabu baada ya kukuta maiti ikiwa haina sanda.
 
Shuhuda wa tukio hilo Abdallah Shaban ambaye ni ndugu wa marehemu ambaye pia ni Mwenyekiti wa SACCOS ya Mwangu kijijini hapo alisema, marehemu alizikwa Januari 13, 2014 katika maeneo ya Malalo yaliyopo pembezoni mwa soko la Ilagala lakini na baada ya hapo walipoenda Januari 14, 2014 kwenye eneo hilo kwa ajili ya maziko ya marehemu mwingine walishangaa kuona kaburi limefukuliwa huku maiti akiwa mtupu.
Shabani alisema, tukio hilo ni la kwanza kijijini hapo na kwamba kufukuliwa kwa kaburi hilo kunaonyesha kulifanywa na watu.
Naye baba mdogo wa marehemu, Issa Salum alisema, tukio hilo ni la mwaka kijijini hapo ambapo polisi wa Kituo cha Ilagala waliamuru kufukua kaburi lote na kukuta maiti tupu pasipo sanda na waliamua kununua sanda nyingine na kuzika upya.
Kutokana na tukio hilo inadaiwa kuwa mama wa marehemu Mwatano Juma alipoteza fahamu baada ya kushuhudia tukio hilo na baada ya kuzinduka hakuweza kuongea chochote kutokana na mshangao alioupata juu ya tukio hilo.
Kamanda mwandamizi msaidizi wa polisi Mkoani hapa, ASCP Frasser Kashai adai hana taarifa zozote kuhusiana na tukio hilo. Marehemu Juma Nkuru Muha (18), alifariki katika Hospitali ya Maweni akisumbuliwa na ugonjwa wa mapafu.

No comments:

Post a Comment