watuhumiwa kuvusha wahamiaji haramu
Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe.
Kamanda wa Polisi wa Viwanja vya Ndege, Seleman Hamis anasema taarifa hizo ni za kushtua kwani hakudhani kama mambo kama hayo yanaweza kutendeka kwani ulinzi mkali umewekwa uwanjani hapo.
Polisi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Dar es Salaam, wanatajwa kuwa wahusika wakuu wa kusaidia wahamiaji haramu kuingia nchini, kinyume cha sheria.
Septemba mwaka jana, mfanyakazi wa Wakala wa Ndege
za Serikali, Dominic Bomani alimwambia Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison
Mwakyembe alipotembelea uwanjani hapo kuwa wapo wahamiaji haramu ambao
wamepewa nafasi nyeti za ajira katika uwanja huo. Dk Mwakyembe aliahidi
kufuatilia suala hilo.
Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa polisi katika
baadhi ya viwanja vya ndege wamejenga mtandao na watumishi wengine,
wakiwamo wa Idara ya Uhamiaji ambao huwawezesha raia wa kigeni hasa
kutoka nchi za Ethiopia, Somalia na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo
(DRC), kuingia nchini bila ya kuwa na nyaraka zinazokubalika kisheria.
Tukio la karibuni zaidi ni lile la kuingizwa
nchini kwa raia watatu wa Pakistani ambao licha ya kukamatwa katika
Uwanja wa Ndege wa zamani (Terminal – I) kutokana na kutokuwa na hati za
kusafiria, wala nyaraka zozote zinazowaruhusu kuingia nchini, baadaye
waliachiwa na kuingia nchini katika mazingira ya kutatanisha.
Chanzo chetu uwanjani hapo kilisema: “Hawakuja na
hati za kusafiria wala nyaraka zozote na waliachiwa huru katika
mazingira ya kutatanisha.”
Chanzo hicho kiliwataja Wapakistani hao kuwa ni
Hussein Amir, Ahmad Tahmir na Shakeel Muhamadadi ambao walifika nchini,
Oktoba Mosi, 2013 saa kumi na moja jioni kwa ndege ndogo ya kukodi
ambayo ilikuwa ikitokea Zanzibar.
Baada ya kufika, walishukia Terminal 1 na baadaye
kwenda kuswali katika msikiti wa karibu, lakini kabla ya kutimiza azma
yao hiyo, walikamatwa na polisi kisha kufunguliwa hati ya kukamatwa (RB)
namba JNIA/1005/2013.
Mapema baada ya kuwasili kwao, wageni hao
walipokewa na Dereva Teksi, Shami Maringo ambaye alikiri kwamba
aliagizwa kuwapokea, lakini kabla ya kuanza safari waliomba kwenda
msikitini kuswali kwa sababu ilikuwa tayari ni saa 12:00 jioni.
Maringo alisema aliwapokea raia hao watatu baada
ya kupewa majina yao na Mtanzania mwenye asili ya Asia ambaye alimwambia
baada ya kuwapokea awapeleke Kariakoo.
“Nilipewa majina matatu kwenye karatasi na mhindi
mmoja, nikaambiwa hao watu watafika saa 10 jioni. Walipofika
nikawatambua lakini tulikamatwa,” alisema Maringo.
Maringo pia alikamatwa na kuambiwa kuwa ataachiwa baada ya mtu aliyemwagiza kuwapokea raia hao atakapofika.
Alisema siku ya pili asubuhi, mtu huyo ambaye hata
hivyo, alisema hamfahamu kwa jina, alifika polisi na Maringo pamoja na
raia hao waliachiwa huru. Maringo anasema hakuweza tena kuwapeleka kwa
sababu gari lake lilipata pancha.
No comments:
Post a Comment