Raia wa Kenya bado wana hofu na mchanganyiko wa kuhama kutoka matumizi
ya teknolojia ya utangazaji ya analojia na kuhamia teknolojia ya
digitali.
Kuingia teknolojia ya digitali Kenya ni kitendawili.
Ifikapo mwaka 2015, muda ambao umepangwa na Umoja wa Mawasiliano ya
Kimataifa Duniani kutawsitisha utangazaji wa kutumia analojia. Kuhamia
teknolojia ya digitali kunalenga kuwapa huduma bora watumiaji, ingawa
kwa nchi za Afrika Mashariki zoezi hilo limekuwa gumu na hivyo serikali
husika kulazimika kuahirisha mara kadhaa.
Huku kesi ya kupinga uamuzi wa serikali wa kuvikatalia leseni ya
matumizi ya digitali vyombo vya habari nchini Kenya haijamalizika, kesi
ambayo ilifunguliwa na wamiliki wa vyombo vikuu vya habari nchini humo
bado kuna masuala yaliyoibuka juu ya kuhamia tekenolojia ya digitali,
ikiwa ni pamoja na malalamiko juu ya wachina kuchukua fursa kubwa ya
kutawala vyombo vya habari, hasa kuelekea teknolojia ya digitali.
Lakini kwa Javas Bigambo, mchambuzi wa masuala ya siasa nchini Kenya,
aliyebobea katika masuala ya vyombo vya habari , utawala na sera
ameliambia shirika la habari la IPS kuwa halikuwa suala la bahati mbaya
kwa serikali kuipa leseni ya digitali kampuni ya Kichina na kuwanyima
wazawa, huku miundo mbinu ya kuanza kutumia digitali ikiwa bado
haijatengenezwa.
Anasema mchambuzi huyo na hapa namnukuu "ikiwa bado tuna majonzi ya
uamuzi wa Bunge kupitisha muswada tata kuhusu vyombo vya habari nchini
humo wenye lengo la kudhibiti tasnia ya uandishi habari nchini bado
serikali inaendelea kuyumbisha uhuru wa vyombo vya habari kwa hali ya
juu", mwisho wa kumnukuu.
Walalamikia kampuni ya Kichina kupewa leseni
Kwa leseni hiyo, kampuni ya Kichina inayomilikiwa na mtandao wa
Pan-Afrika –PANG na SIGNET-shirika la kimataifa la utangazaji , watakuwa
na jukumu la kuwaunganisha watumiaji wa televisheni na televisheni hizo
, ambapo pande zote zitahusika katika kurusha matangazo kwa makubaliano
maalum na wamiliki wa vyombo vya habari, ambapo televisheni za ndani
zitawajibika katika kutayarisha matangazo pekee.
Kwa upande wake Alex Gakuru ambaye ni mwenyekiti wa chama cha watumiaji
wa mawasiliano ya teknolojia nchini Kenya na mjumbe wa kamati ya
kusimamia uhamiaji kutoka analojia kwenda digitali amesema kumekuwa na
hali ya wasi wasi kuwa kampuni hiyo ya kichina itadhibiti vyombo vya
ndani vya habari na hivyo kudharau katiba na sheria za nchi, ingawa
anasema hofu hizo zinapata ushawishi mbaya.
Amesema mawasiliano kwa umma ni suala la kisheria kwa mamlaka za
mawasiliano na vyombo vya habari na kwamba kampuni hiyo ya kichina
itakuwa na mamlaka ya kusambaza ving'amuzi vyenye kuonyesha chaneli zote
cha televisheni za ndani na si kupendelea chaneli fulani,ikiwa itafanya
hivyo itajiweka katika hatari ya kufungiwa leseni yake.
Grace Githaiga mdau wa mtandao wa mawasiliano ya teknolojia Kenya
anasema kuwa ingawa kamisheni ya mawasiliano Kenya na mamlaka
inayosimamia mawasiliao wamedai kuwa vyombo vya habari vya ndani
hawakupata zabuni ya leseni ya digitali, hata hivyo vyombo hivyo vina
kila sababu ya kulalamikia usimamizi wa kampuni ya kigeni wa digitali
kwa kuwa wanaona wamevunjiwa haki yao.
Hata hivyo amasema wasi wasi juu ya kampuni hiyo ya Kichina
kupewa leseni limetiwa chumvi kutokana na ukweli kwamba makamupni ya
simu yanatumia tekenolojia ya kichina huku mamilioni ya watu wakiendelea
kutumia vifaa vya umeme vinavyotengezwa au kununuliwa kutoka China.
Takwimu zilizotolewa na serikali zinaonyesha kuwa, shirika la habari la
utangazaji la China, Xinhua husambazwa habari kwa watu milioni 17
wanaotumia simu nchini Kenya.
Lengo la teknolojia ya Digitali inayoendelea kuhimizwa kutumiwa katika
ukanda wa Afrika Mashariki ni kutaka kuendana na kasi ya ukuaji wa
teknolojia ya mawasiliano kote duniani.
Teknolojia ya digitali kuongeza ubora
Miongoni mwa faida za kutumia teknolojia ya digitali ni kuongezeka kwa
ubora wa matangazo, ongezeko la chaneli za televisheni litakalotokana na
matumizi bora ya masafa, kuwepo kwa masafa ya ziada yatakayopatikana
baada ya kuzimwa kwa mitambo ya analojia inayotumia masafa mengi.
Faida nyingine zilizobainishwa ni kuongezeka kwa watoa huduma wa
mawasiliamo ya simu, matangazo ya televisheni kupatikana kwa vifaa vingi
zaidi vya mawasilino kama vile simu za mkononi na kompyuta kupitia
mtandao wa internet.
No comments:
Post a Comment