Friday, 10 January 2014

Waziri Kigoda: Mfumo mashine EFDs ni mbovu, unakandamiza


Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Abdallah Kigoda.

 Asema Serikali inajipanga kutafuta ufumbuzi wa changamoto zilizopo.
  Serikali imekiri mfumo wa ulipaji kodi na ule wa utumiaji wa mashine za kutolea risiti(EFDs) kuwa ni mbovu na hivyo unahitaji kufanyiwa kazi.


Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Abdallah Kigoda, amesema mfumo wa ulipaji kodi nchini bado unakabiliwa na matatizo ambayo hayawezi kusaidia katika kumuendeleza mfanyabiashara zaidi ya kumkandamiza.
Dk Kigoda alisema hayo wakati alipokutana na wafanyabiashara wa mikoa yote nchini, kuhusu maboresho katika ukusanyaji wa mapato yatokanayo na kodi na tozo mbalimbali wanazotozwa wafanyabiashara, wajasiriamali na mapendekezo ya uendeshaji wa biashara nchini.
Alisema baada ya serikali kulitambua hilo hivi sasa inajipanga kutafuta ufumbuzi utakaosaidia kumaliza changamoto hizo. Hata hivyo, bado kuna kazi kubwa ya kupata mfumo bora wa uendeshaji biashara na ulipaji kodi.
“Suala la mashine za kutolea stakabadhi mmelizungumzia kwa mapana, lakini hata hivyo bado zina changamoto lakini haya yote mliyoyazungumza wakati nikienda kukutana na wenzangu endeleeni na kufanya biashara zenu kwa utaratibu wenu wa zamani hadi ufumbuzi utakapatikana,” alisema Dk Kigoda.
Dk Kigoda alisema kama mtakumbuka kuna taarifa zilizowahi kutolewa na vyombo vya habari kimataifa kuwa Tanzania ilikuwa ni moja ya nchi iliyofanya vibaya katika kipindi cha mwaka jana kutokana mfumo mbaya uliosbabishwa na sababu mbalimbali ikiwamo masuala ya ukusanyaji kodi.
Aidha, aliwataka kuwa wavumilivu wakati matatizo yao yakishughulikiwa kwani watambue matatizo ya kiuchumi hayatatuliwi kwa migomo, maandamano ya kisiasa bali hutatuliwa kiuchumi.
“Tanzania tuna tatizo kubwa sana na lazima tuliondoe hili siyo lingine bali ni kutoaminiana kati ya serikali na wafanyabiashara. Hili lazima tulitatue kwa sababu serikali tunaona wafanyabiashara ni wajanja wanaweza kukwepa kodi wakati wafanyabiashara nao hivyo hivyo….” alisema na kuongeza:
Huku akishindwa kuweka wazi akiepuka kulizungumzia kwa undani suala la EFD, zaidi akiwapongeza wafanyabiashara hao kwa kauli yao kuwa hawapingi kulipa ko.iN Aliwasihi suala hilo litakwisha baada ya kikosi kazi kitakachoundwa kikiwashirikisha wafanyabiashara hao.
“Hatuwezi kumkamua ng’ombe atoe maziwa bila kumpa majani na hatuwezi kumaliza matatizo ya uchumi kwa maandamano au kuwasikiliza wanasiasa. Njia pekee ya kutatua matatizo haya ni kushirikisha wataalamu wa uchumi” aliongeza.
Dk Kigoda alisema waraka uliotolewa na wafanyabiashara utafanyiwa kazi na haki itatolewa baina ya mfanyabiashara mkubwa, wa kati na mfanyabiashara mdogo
Alisema serikali itaunda kikosi kazi kitakachoshirikisha jumuiya hiyo ya wafanyabiashara ili waweze kuwekeza katika mazingira mazuri.

No comments:

Post a Comment