Naibu Waziri wa Sheria na Katiba, Angellah Kairuki amesema kuwa Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 iko kwenye mchakato wa kurekebishwa kutokana na utata unaokinzana na sheria nyingine za masuala ya kijinsia.
Akizungumza baada ya ufunguzi wa warsha ya siku
moja ya waandishi wa habari na sheria na sera zinazohusu ukatili wa
kijinsia iliyoandaliwa na Taasisi ya Champion na Engender Health
wilayani Bagamoyo juzi, Kairuki alikiri kuwepo kwa utata wa sheria hiyo
jambo linaloendelea ukatili hasa kwa wanawake.
“Utata wa sheria ya ndoa ya mwaka 1971 ulijadiliwa
katika Baraza la Mawaziri na walishafika mbali. Lakini ilionekana kwa
kuwa masuala ya ndoa na mirathi yanagusa mila, desturi, dini na tamaduni
za watu, ilionekana siyo rahisi kutunga sheria haraka,” alisema Kairuki
na kuongeza:
“Wapo wanaosema mtoto hawezi kuolewa akiwa na
miaka 14 na wapo wanaosema anaweza. Baraza la Mawaziri liliamua kuwa
kuwe na kura ya maoni (white paper).”
Hata hivyo alisema kuwa wakati mchakato huo
ukikaribia kuanza uliingiliana na mabadiliko ya Katiba. Hivyo alisema
kura hiyo ya maoni itafanyika baada ya kupatikana kwa Katiba Mpya.
Awali akifungua warsha hiyo, Kairuki alisema kuwa
Serikali imechukua hatua za kukabiliana na ukatili wa kijinsia ikiwa
pamoja na kuanzisha dawati la jinsia na watoto kupitia Jeshi la Polisi
na timu za ulinzi na usalama wa watoto kupitia Idara ya Ustawi wa Jamii.
Akitoa mada katika warsha hiyo, Mkurugenzi
Msaidizi wa Taasisi ya Engender Health, Dk Monica Mhoja alisema Serikali
ya Tanzania inasifika kwa kuridhia sheria na mikataba ya kimataifa
kuhusu ukatili wa kijinsia, lakini hazitekelezwi ipasavyo.
“Tunapokuwa kwenye majukwaa ya kimataifa, Tanzania
tunasifika kwa kuridhia sheria na sera nyingi, wanapotuhoji kuhusu
utekelezaji inakuwa shida,” alisema Dk Mhoja.
No comments:
Post a Comment