Dar es Salaam. Watu wawili wamefariki dunia katika tukio
lililokuwa na mwendelezo, mmoja akimchinja mtoto na yeye kuuawa kwa
kupigwa mawe na wananchi wenye hasira.
Polisi walithibitisha mauaji hayo ya kutisha na
kueleza kuwa yalitokea juzi saa 12 jioni maeneo ya Mbagala Charambe
Foma, jijini Dar es Salaam, ambapo katika tukio la kwanza Mohamed Said
(36), alimkamata Jamal Salum (12) aliyedaiwa kuwa mwanafunzi wake na
kumchinja kama kuku.
Habari zinaeleza kuwa Said akiwa nyumbani kwake
alimkamata Jamal ambaye alikuwa mwanafunzi wa darasa la tano katika
Shule ya Msingi Nzasa na kumlaza chini, kisha akamchinja.
Hali hiyo inaelezwa kuibua hasira za wananchi
wenye hasira na kuvamia nyumbani kwa Said na kumpiga mawe hadi naye
kupoteza uhai wake.
Mkuu wa Upelelezi, Wilaya ya Kipolisi Mbagala, ASP
Walelo, alieleza kuwa siku ya tukio (Juzi), Jamal alikuwa na mwenzake
Ramadhani Salum (11) ambaye ni mwanafunzi wa darasa la nne, Shule ya
Msingi Kichechem aliyemsindikiza Jamal katika nyumba ya Said ambapo
mjomba wake amepanga na walipokuwa wakitoka wakakutana na Said, ambaye
alimshika Jamal, akamlaza chini na kumchinja kwa kutenganisha kichwa na
kiwiliwili.
“Wakati akimchinja, Ramadhani akakimbia kutoa
taarifa kwa watu waliokuwa karibu, walipofika walikuta tayari Salum
ameshachinjwa,” alisema Walelo na kuongeza:
“Baada ya hapo, wananchi wenye hasira walivunja
mlango wa nyumba ya Said na kumkuta akiwa ameshika kisu alichofanyia
mauaji na kumpiga hadi kupoteza maisha.”
Alifafanua kuwa Said, anafanya kazi katika Shule ya Al-nur-al iliyopo Charambe Foma na kwamba alikuwa ni mwalimu wa madrasa.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Charambe, John Bazil, alisema kuwa anadhani Said alikuwa na matatizo ya akili.
“Nimehamia hapa juzi juzi, sifahamu sana, lakini
taarifa nilizokuwa nazo ni kwamba, Said ana matatizo ya akili ambayo
humjia na kuondoka, kitu ambacho watu waliokuwa wakiishi naye walikuwa
wanakiona cha kawaida kwa kuwa walimkuta akiwa hivyo,” alisema Bazil.
No comments:
Post a Comment