Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wakinyoosha mikono ili wapatiwe Rasimu ya Kanuni zitakazoendesha bunge hilo
Madai ya Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kutaka nyongeza ya posho ya vikao vya Bunge hilo yamegonga mwamba, Mwananchi limebaini.
Habari kutoka ndani ya kamati iliyoundwa na
Mwenyekiti wa Muda wa Bunge la Katiba, Pandu Ameir Kificho ili
kufuatilia madai hayo, zimedai kuwa baada ya uchunguzi wa kina, wajumbe
wa kamati hiyo hawakuona sababu ya kupendekeza posho hizo kupandishwa.
Taarifa hizo zilidai kuwa wajumbe hao wamefikia
uamuzi huo baada ya kupitia viwango vya posho vinavyolipwa na Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali na Mashirika ya Umma.
Pia kamati hiyo ilichambua viwango vya posho
walivyolipwa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na viwango vya
posho ya kujikimu vya Sh80, 000 kwa siku wanavyolipwa watumishi wa
Serikali.
“Hili jambo linahitaji busara sana na kutazama
mazingira ya nchi pia, kwa hiyo wajumbe wale baada ya kuoanisha viwango
vya posho vya taasisi mbalimbali wameona Sh300,000 zinatosha,” alisema
mmoja wa wajumbe ambaye hakutaka jina lake kutajwa.
Mjumbe mwingine, ambaye pia hakutaka kutajwa,
alisema kuwa watakaa leo kukamilisha taarifa ya utafiti wao, kabla ya
kuikabidhi kwa Mwenyekiti Kificho.
Alisema pamoja na umuhimu wa kazi za mbunge,
lakini isingekuwa rahisi kuongeza posho katika mazingira ya sasa, ambapo
wananchi wanalia hali ngumu ya maisha.
Wajumbe hao walioteuliwa na Mwenyekiti wa Muda wa
Bunge Maalumu, Pandu Ameir Kificho ni William Lukuvi, Mohamed Abood
Mohamed, Freeman Mbowe, Paul Kimiti, Jenister Mhagama na Asha Bakari.
Awali, taarifa kutoka ndani ya Bunge zilidokeza
kuwa wajumbe hao walikuwa wakutane jana saa 9:00 alasiri ili kuandaa
ripoti itakayopelekwa kwa Kificho ikiwa imebeba ushauri kuwa kiwango cha
sasa cha posho kinatosha.
Sh300,000 wanazolipwa wajumbe wa Bunge Maalamu la
Katiba zinajumuisha Sh80,000 kwa siku ambayo ni posho ya kujikimu na
Sh220,000 kwa siku kama posho maalumu ya kuhudhuria kikao.
Posho maalumu ya Sh220,000 inajumuisha posho ya
dereva inayopaswa iwe kati ya Sh40,000 na Sh45,000 kwa siku, usafiri wa
ndani (mafuta ama teksi), mawasiliano na matumizi mengine binafsi.
Alipoulizwa kuhusu jambo hilo mmoja wa makatibu wa Bunge hilo,
Yahya Khamis Hamad alisema suala la posho linashughulikiwa na Serikali.
“Ninachokifahamu ni kuwa suala la posho limetoka
mikononi mwa Kificho na sasa lipo serikalini. Kamati iliyoundwa bado
inalishughulikia suala hilo. Hicho ndiyo ninachokifahamu,” alisema Hamad
ambaye pia ni Katibu wa Baraza la Wawakilishi.
Kwa nyakati tofauti gazeti hili lilimtafuta
Kificho, Waziri wa Fedha na Uchumi, Saada Mkuya kuzungumzia suala hilo,
lakini simu zao za mkononi zilikuwa zikiita bila majibu.
Hoja ya kutaka nyongeza ya posho iliibuliwa na
wajumbe wawili ambao ni wabunge wa CCM waliodai kuwa kiwango cha
Sh300,000 wanacholipwa, hakitoshi kwa kile walichodai kuwa ni kuishi
Dodoma ni gharama kubwa.
Hata hivyo uchunguzi wa kina umebaini kuwa baadhi
ya wajumbe wanaishi katika hoteli za kati ya Sh20,000 na Sh40,000 kwa
siku huku baadhi yao wakiishi katika hosteli kwa Sh8,000 kwa siku.
Mmoja wa wajumbe, Augustino Mrema alidai kuwa
baadhi ya wajumbe wanataka kuligeuza Bunge hilo ‘shamba la bibi’ kwa
kudai posho zaidi kwa kisingizio cha kupanda gharama za maisha.
Mrema alisema kiasi cha Sh300,000 wanacholipwa
wajumbe kinatosha kwani zipo hoteli nzuri za kati ya Sh15,000 hadi
Sh40,000 ambazo zina hadhi na sifa ya kuishi wajumbe wa Bunge la
Katiba.
“Mjumbe ameamua kwenda kuishi chumba cha Sh200,000
wakati akijua atalipwa posho ya Sh300,000 halafu analalamika kupanda
kwa gharama za maisha, hizi gharama zimetengenezwa,” alisema Mrema.
Alisema gharama za teksi kutoka bungeni hadi
maeneo ya Area C na D haizidi Sh12,000 wakati chakula kinaanzia Sh6,000
hadi Sh20,000 na kuhoji iweje Sh300,000 zionekane hazitoshi.
Hoja ya baadhi ya wajumbe kudai posho zaidi
imepigiwa kelele nchi nzima huku wananchi wakimtaka Rais Jakaya Kikwete
kulivunja Bunge hilo, kama wataendelea kung’ang’ania kupanda kwa posho.
Mjumbe mwingine wa Bunge hilo ambaye pia ni Naibu
Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro ameahidi kuanzia leo kukusanya saini
za wajumbe wanaopinga suala hili ili ampelekee Rais Kikwete kama
ushahidi.
No comments:
Post a Comment