Mpenzi
msomaji wangu, ikiwa huna kawaida ya kumshukuru Mungu, anza leo hii na
faida zake utaziona. Hata katika uhusiano wako, unapomtanguliza Mungu
katika kila kitu, atakuongoza na kukufanya mwenye furaha siku zote. Hii
si simulizi ya kusisimua ya kitabu ni ukweli ambao upo wazi na kama
ukichukua hatua utauona.
Katika
uhusiano na mapenzi umakini wa hali ya juu sana huhitajika ili uweze
kuwa bora kila siku na kuufanya uhusiano wako kuwa wenye nguvu na
usiotetereka! Katika hili hutegemea zaidi jinsi unavyoendesha uhusiano
wako.
Ukitaka mpenzi wako akuchoke au umchoke, wewe
ndiye mwamuzi, lakini pia ukitaka mpenzi wako asikuchoke au usimchoke
wewe ndiye mwenye uamuzi kwa kuwa una uwezo wa kuyafanya yote hayo.
Wengi
wanakuwa hawaelewi kuhusu hili, anaingia kwenye ndoa na mke wake au
mumewe lakini baada ya muda anajikuta mapenzi yakipungua siku hadi siku
mpaka anafikia hatua ya kuwa na mwanaume mwingine nje ya ndoa yake au
kama ni mwanaume anaamua kuwa na nyumba ndogo! Hayo yote nayaita ni mambo ya kujitakia!
Inawezekana
ukaendelea kuwa bora kwa mpenzi wako, inawezekana mpenzi wako
akaendelea kuwa bora kwako ikiwa utahitaji kufanya hayo kwa dhati.
Hakika kama ukitaka unaweza kuendelea kuwa wa kisasa katika uhusiano
wako. Yapo mambo mengi sana ya kufanya ili uhusiano wako usitetereke.
Katika mada hii nimekuandalia mambo 10 muhimu ambayo ukiyazingatia kwa
umakini mkubwa uhusiano wako utakuwa imara siku zote. Kwa ufafanuzi
zaidi, hebu fuatana nami katika vipengele vifuatavyo, naamini utaingiza
kitu kipya ubongoni mwako.
MWANZO WA PENZI LENU!
Siku
zote nimekuwa nikisisitiza kuwa, jinsi unavyoanza ndivyo
utakavyomaliza! Waswahili hawakuishia hapo, wakaongeza kuwa; ‘Unavuna
kile ulichopanda!’. Naamini katika semi hizo kuna mambo umejifunza. Kama
ulianza vibaya uhusiano wako tegemea kumaliza vibaya, lakini kama
ulinza vizuri basi tarajia maisha mazuri ya kimapenzi yasiyo na maumivu
katika moyo wako.
Kama
unatarajia kuingia katika uhusiano na mpenzi mpya hakikisha hujionyeshi
tofauti na hali yako halisi ilivyo! Jifunze kujikubali, hata kama
unafanya kazi ambayo unadhani ni hadhi ya chini, mbainishe mpenzi wako
hali halisi ilivyo. Kama anakupenda, kazi yako haiwezi kupunguza mapenzi
baina yenu.
Ikiwa
ndiyo kwanza mnaanza uhusiano, zingatia hili, na kama mpo katika
uhsiano kwa muda mrefu ukagundua wazi kuwa kuna mahali ulikosea, anza
kufanya mabadiliko kuanzia sasa. Bado hujachelewa ndugu yangu.
Kudanganya
hakuna mantiki, kudanganya ni utumwa, usikubali kuingia katika utumwa
au kifungo cha aina hiyo. Ngoja niwape kisa cha rafiki yangu mmoja; jamaa
alimdanganya mpenzi wake anafanya kazi katika shirika fulani kama
kiongozi, akamwongopea kuwa mshahara wake ni mkubwa na mambo mengine
mengi!
Yote hayo ilikuwa ni kumfanya mpenzi wake amuamini na kumpenda, akilini mwake akiamini pesa ndiyo mhimili wa mapenzi.
Kwa
kuwa mpenzi wake alijua bioyfriend wake ana kazi na mshahara mzuri,
alikuwa akimsumbua jamaa kila kukicha akafanyiwe shopping! Kilichotokea
hapo ni kwamba jamaa alikuwa akimkwepa kila kukicha. Unajua kwanini
alikuwa akimkwepa? Sababu ya pesa! Kama asingesema uwongo usumbufu wote
alioupata asingeupata.
Jifunze
kujikubali ulivyo, usitake kujionyesha kwa watu upo katika hadhi fulani
wakati hali halisi haipo hivyo, huo ni ulimbukeni ambao unatakiwa
kuushinda! Ukweli ni silaha ya kwanza katika mapenzi, anza hivyo kuanzia
mwanzo na kama ulikosea, ulijisahau au hukujua, basi anza leo!
JIPENDE NA KUJITHAMINI...
Itakuwa
kichekesho kama utasema unampenda mpenzi wako wakati wewe mwenyewe
hujipendi! Huwezi ukasema unamthamini mpenzi wako wakati thamani yako
mwenyewe huitambui.
Naamini tunakwenda sawa, kama unashindwa hata kuoga na kubadilisha nguo safi nani atakayekupenda? Huwezi
kuwa wa kisasa kama huzingatii usafi, hakuna atakayevutiwa na wewe kama
wewe hutaki kujivutisha. Sio ajabu mpenzi wako akakutosa kwa sababu tu
huna muonekanano mzuri kwa rafiki zake.
Nani
atakayekupenda wakati wewe mwenyewe huonyeshi kama unajitambua? Utakuta
mwingine anajichukia bila mwenyewe kujua anajichukia! Unaweza ukamkuta
mtu anajitoa kasoro mwenyewe, mara mimi mweusi sana mara mimi mweupe
sana, miguu yangu imekaa upande, kwa nini nisingezaliwa kama fulani na
maneno mengine yanayofanana na hayo. Amini ulivyoumbwa hakuna makosa
yoyote, jinsi ulivyoumbwa unapaswa kuwa kama ulivyo.
Jikubali,
jithamini! Kuwa msafi wakati wote, kauli zako ziwe safi siku zote
mpenzi wako atakuwa huru kuwa na wewe. Isifikie hatua mpenzi wako
akataka kutoka na wewe lakini akasita kwasababu hajui ukija utakuwa
umevaa nguo za namna gani. Upo hapo?
No comments:
Post a Comment