Friday, 14 February 2014

MWANAMKE! UKIMPA SHOGA YAKO UPENYO KWA MPENZI WAKO ITAKULA KWAKO

Unapokuta mwanamke au mwanaume anamlaumu mume au mke wake kwa kitendo chake cha kukaa na kuzungumza na mtu wa jinsia nyingine mara kwa mara utasemaje, je utasema ni wivu uliopitiliza?

Inawezekana ikawa ni wivu, lakini kwa upande wa pili, huenda haitokani na wivu, bali ukweli kwamba, watu wawili wa jinsia mbili wanapozoeana katika kuzungumza, hatimaye uwezekano wa kukutana kimwili hujitokeza.


Kwa kupitiwa au kujisahau, wanawake wengi huwa wanawapa nafasi marafiki au shoga zao kuwa karibu na waume zao kwa kuzungumza, wakiamini kwamba, kuzungumza tu, hakuwezi kuwa na madhara. Huku ni kujidanganya kwa kiasi kikubwa.


Kwa kadiri watu wa jinsia mbili wanavyozoeana katika kuzungumza na hasa wanapoanza kuzungumzia mambo yao ya ndani, ndivyo ambavyo mipaka huvukwa na kujikuta wakihusiana kimwili.


Pale mpenzi kuwa karibu mara nyingi na mtu mwingine wa jinsia tofauti kwa maelezo kwamba, ‘ni rafiki tu,’ ujue tatizo liko karibu kuanza kama halijaanza. Kuwa karibu sana kwa mazungumzo mara kwa mara na mtu wa jinsia nyingine, ni aina ya uzinzi pia, kutegemea tu aina ya mazungumzo.


Labda nijaribu tu kuwasaidia wale ambao wako kwenye uhusiano tayari. Wanapohisi dalili fulani, kuhusiana na rafiki zao wa jinsia tofauti, wanapaswa kujua kwamba, hivi karibuni, urafiki huo utaisha na watakuwa wapenzi. Kama hawataki kuharibu uhusiano waliomo, wanapohisi dalili hizi wanapaswa kujitoa.


Kama mtu ana rafiki wa jinsia tofauti, ambaye siku zote amekuwa akijiambia ni marafiki tu, anapojikuta ameanza kumwotea ndoto za mchana kama za Alinacha, ni hatari. Kumwotea ndoto za mchana rafiki wa jinsia tofauti si dalili nzuri hata kidogo na haiashirii jambo jema huko mbeleni.


Kama mwanaume ana rafiki wa jinsia tofauti na anapokuwa na jambo au mambo ya kutaka mtu mwingine ayasikie ili ahisi nafuu, anayaweka kwa ajili ya rafiki huyo, badala ya kumwambia mkewe, urafiki huo utageuka balaa sasa hivi. 


Kuna wanaume ambao hata kama ametaka kugongwa na gari, hatazungumza jambo hilo na mkewe, bali atangoja akikutana na huyo rafiki yake wa jinsia tofauti ndiyo amweleze. Hata kama mwanaume huyu hajashiriki tendo la kujamiiana na rafiki huyo, uwezekano ni kwamba, bado kitambo kidogo watashiriki.


Mwanaume anapoona na kuamini kwamba, rafiki yake wa jinsia nyingine anamwelewa vizuri zaidi kuliko mkewe, ni wazi kabisa kwamba, hiyo ni hatari, kwani ni safari ya moja kwa moja kuelekea kushirikiana kimwili.



Kama imefikia mahali ambapo mume anashiriki kujadili siri za mke wake na rafiki wa jinsia nyingine ni dalili mbaya kwamba, watu hao kama hawajaanza kushirikiana kimwili, wataanza muda mfupi ujao.


Mwanaume kuanza kumnunulia rafiki wa jinsia nyingine nguo za ndani, pafyumu, mapambo na vitu vya aina hiyo. Jambo hilo ni ishara kwamba, ile, ‘ni rafiki yangu tu,’ itafutika sasa hivi na watu hao watakuwa wapenzi.


Mwanaume........Kama uko kwenye urafiki ambao una dalili hizo, ni vema kuanza kukagua mwenendo wako na huyo rafiki yako. Kama hutaki kutoka nje ya ndoa yako, inabidi au ujitoe kwenye urafiki huo, au uache kufanya hayo mambo niliyoyaeleza.


Namalizia kwa kuwaambia wanawake kwamba, huna haja ya kumwacha huru shoga yako na mumeo kwa kudhani ni vigumu kwa watu hao kukusaliti. Wakianza kushiriki mazungumzo ya kihisia haraka sana wataingia mahali ambapo watataka kushirikiana kimwili.


Hata wao katika hatua za awali watakuwa hawana lengo la kushiriki tendo la kujamiiana, lakini mazungumzo yao, hatimaye yatawafanya waungane kihisia na kitakachofuata kitakuwa ni maumivu kwako.


Weka mipaka ya makusudi, onesha kutoridhishwa na mume au mpenzi wako ama shoga yako unapoona mmoja au wote wanajisahau na kuanza kuwa karibu sana kimazungumzo.



Suala la ‘shogako leo alipita ofisini kwangu,’ kutoka kwa mume au mpenzi wako, usilikubali kirahisi. Suala la ‘nasikia shemeji anasafiri, naomba anipe lifti, na mie naenda Morogoro,’ usikubali kirahisi. Bora uambiwe una wivu kuliko kuja kupoteza……

No comments:

Post a Comment