Watafiti
( University of Colorado Boulder) wanasema asilimia kubwa ya migongano na mifarakano inasababishwa na
kutokuwasiliana kwa ufasaha kwa wahusika waliopo katika mifarakano au migongano
husika. Na inasemwa pia (Examiner.com) kuwa dawa namba moja ya kuzuia na kusuluhisha
migongano ni kuboresha mifumo ya mawasiliano na kuhakikisha wahusika wanakuwa
na mawasiliano fasaha. Ukiachilia na ukweli huu wa kitafiti, wengi wetu
tumejikuta hatutoi kipaumbele katika kujifunza na kuboresha uwezo wetu wa
kuwasiliana kwa ufasaha. Ikumbukwe kuwa, kumudu kuwasiliana kwa ufasaha, ni
zaidi ya kuweza kusoma na kuandika. Ni zaidi ya kujua misamiati mbalimbali ya
darasani ihusuyo mawasiliano kama vile (receiver, sender, barriers to
communication n.k.). Katika makala hii
tutaangalia mambo ya msingi tunayoweza kuyaboresha katika mawasiliano ili
kuboresha mahusiano yetu, yawe ya kimapenzi, kibiashara au kiofisi.
Ni muhimu kujua maana pana ya Mawasiliano
Fasaha
Maana
pana ya mawasiliano fasaha inatutaka tuchukulia swala la mawasiliano kuwa ni
jambo la kila siku, jambo la kila wakati, hivyo ni swala endelevu ambapo
kulimudu vema, linahitaji maamuzi thabiti ya mtu binafsi kuwa ataishi kwa
kufuata kanuni husika. Ingawa kanuni za mawasiliano fasaha zaweza kuonekana
kama vile ni nadharia, umaana wa
mawasiliano sahihi upo katika kufanya kwa matendo yanayotakiwa kukamilisha
mawasiliano fasaha.
Acha
basi, tuangalie maana pana ya mawasiliano fasaha (kwa kiingereza effective
communication):
Mawasiliano fasaha
ni yale mawasiliano ambayo yanatimiza vigezo vyote vifuatavyo:
- Kigezo namba 1: Mawasiliano ambayo mtoaji ujumbe anaeleweka kama alivyokusudia, na pia mpokeaji ujumbe (receiver) anapokea ujumbe na kuulewa kama ilivyokusudiwa. Ndio maana basi kuna haja ya kujifunza namna bora ya kutoa ujumbe, na namna bora ya kupokea ujumbe.
- Kigezo namba 2: Mawasiliano fasaha yanawezesha lengo kuu la mawasiliano kufikiwa. Mfano kama lengo ni kuomba ruhusa, basi ruhusa inapatikana, isipokuwa pale tuu mazingira mengine nje ya mawasiliano yanalazimisha ruhusa kutokutolewa. Hapa ina maana kuwa sababu kuu ya kutopata ruhusa sio kwakuwa mhusika hakueleweka vema au hakufanya mawasiliano kiufasaha, bali kuna mambo mengine nje ya mawasiliano yanafanya upatikanaji wa ruhusa kusiwe jambo fasaha. Mfano, kuna hali ya hatari kutokana na vurugu.
- Kigezo namba 3: Mawasiliano fasaha yanawezesha hali ya kuelewana hata baada ya mawasiliano kukamilika. Kigezo hiki kinamaanisha kuwa lengo sio tuu kufanikiwa kupata unachohitaji lakini pia uchukulie maanani jinsi unayosema au kuandika yanavyoweza kuathiri uhusiano wako wa sasa au wa baadae na huyo unayewasiliana naye.
Jinsi ya kufanya mawasiliano
fasaha
Ili kufanya mawasiliano fasaha kuna mambo 10 muhimu ya kuzingatia.
Mambo haya yanaelezwa hapa:
- 1.Tambua uhusiano wako na mpokeaji wa ujumbe: Hii inamaanisha kuwa tambua unawasiliana na nani , na kwamba wewe ni nani kwa huyo mhusika, na huyo mhusika ni nani kwako. Mfano, utasikia wapenzi wengi wamejikuta wapo katika mzozo kwakuwa tuu mmoja amehisi kudharauliwa kwa vile mwenza wake alivyomjibu, au alivyomueleza jambo fulani. Utasikia “ kwanini uzungumze hivyo kama vile mie sio mkeo?” au “ Kwanini uzungumze hivyo kama vile hujui unazungumza na mumeo?”
- Tambua hali ya kiakili aliyonayo mpokeaji wa ujumbe: Hii inamaanisha kuwa kabla ya kuwasiliana na mhusika fulani fanya kautafiti walau kadogo kujua kwa kiasi gani mhusika yupo tayari kiakili kupokea kile unachotaka kuwasiliana naye. Si ajabu kukuta mwanadada analalamika kuwa mpenzi wake hakutimiza alilohitaji au hakuonyesha kujali alipokuwa anazungumza naye, wakati kiukweli mwanaume alikuwa ‘bize’ anaangalia mpira. Akili yake yote ilizama huko. Mambo yanayoweza kufanya akili isiwe tayari au isiweze kupokea mawasiliano kwa ufasaha ni kama vile mtu akiwa na hasira, mtu akiwa amechoka, mtu akiwa na mawazo, mtu akiwa na hofu, au huzuni, n.k
- Tambua utamaduni wako na utamaduni wa mhusika unayewasiliana naye: Hapa neno utamaduni linamaanisha namna ya kuishi ya mtu fulani, mfano vile mtu anavyoamini katika mambo fulani, vile mtu anavyopenda kuonekana mbele za watu, vile mtu anavyosalimiana na wengine n.k. Ni muhimu kutambua hivi na kujua namna ya kufanya mawasiliano kiasi kwamba utamaduni wa mtu hauathiri kuelewana kwenu, na mahusiano yenu baada ya kuwasiliana. Mfano, waweza simama wakati unamsalimia mkwe, ila kwa utamaduni wa mkwe, ulitakiwa upige magoti, hivyo hata baada ya kuondoka kwako, utaacha gumzo kuwa hauna heshima. Tayari hii itapelekea kutokuelewana kati yako na upande wa ukweni. Hali kadhalika , kama unayewasiliana naye ni mteja, halafu ukafanya kinyume na matarajio yake ni kwamba utajikuta umepoteza mteja. Zingatia mawasiliano yasiyotumia maneno: Kumbuka kwamba mbele ya watu wengine tunajikuta tunatoa ujumbe fulani kwao hata kama hatuelezi kwa maneno ujumbe husika. Mambo kama vile kuguna, kurembua macho, kuangalia pembeni, kuziba masikio, n.k yote yanatoa ujumbe fulani kwa mtu mwingine. Tatizo la aina hii ya utoaji ujumbe ni kuwa , kwakuwa hakuna maneno, basi mpokeaji wa ishara husika anaweza kuwa na tafsiri tofauti na unachokusudia. Mfano, unaweza kukuta mtu analalamika “ Kwa nini unanikaripia?” wakati kiukweli haukudhamiria kumkaripia, bali jinsi ulivyokuza sauti yako, mwingine ameelewa kuwa umekasirika. Hii pia inaweza kuchangiwa na namna unavyoonekana, pengine unazungumza huku umekunja sura.
- Dhibiti vizuizi vya mawasiliano (barriers to communication): Hakikisha wakati wote unapotaka kuwasiliana na mtu kuwa mtu huyo ametoa usikivu wa kutosha kwako au yupo na utayari wa kuwasiliana nawe ili kwamba unachotaka kukiwasilisha kwake kieleweke vema. Si ajabu kukuta mtu akilalamika kuwa mwenza wake hakufanya jambo fulani, eti kaonyesha dharau kwa kutokufanya hivyo, wakati ukweli ni kuwa mwenza huyo, wala hakuupata ujumbe husika. Au wakati ujumbe unamfikia hakuwa katika hali ya kumuwezesha kutilia maanani ujumbe husika. Mfano wa vizuizi vya mawasiliano ni kama vile, makele, lugha unayotumia kuwasiliana na mwenzako pengine asiielewe vema – mfano ,umetumia vifupi vya maneno mengi, au umechanganya sentensi kiasi kwamba ujumbe kamili haueleweki vema, n.k
No comments:
Post a Comment