Dar es Salaam. Tahadhari imetolewa kwa wazazi kuwa makini na
vyakula wanavyokula watoto wao kufuatia kuibuka kwa mbinu mpya ya
wauzaji dawa za kulevya kuweka dawa zao hizo kwenye vyakula
vinavyopendwa na watoto.
Akihutubia kwenye mkutano wa Baraza la Vijana wa
Wilaya ya Temeke, Mbunge wa Jimbo la Kigamboni, Dk Faustine Ndugulile
amesema, wauzaji wa dawa za kulevya kila siku wamekuwa wakibuni njia
mpya za kuhakikisha wanapata kundi kubwa la watumiaji wa dawa hizo.
Katika kuhakikisha dhamira yao hiyo inatimia, hivi
sasa wamebuni njia mpya ya kuweka dawa hizo kwenye vyakula vidogo
vidogo vinavyopendwa na watoto kama vile kashata na ubuyu.
“Ni jukumu letu sote pamoja na nyinyi vijana ni
kuelekeza nguvu zetu katika mapambano ya dawa za kulevya kwani, kwa sasa
yanaonekana kuwa janga la kitaifa kutokana na kuathiri nguvu kazi kubwa
ya taifa letu,” alisema.
Amesema takwimu za kitaifa za matumizi ya dawa za
kulevya kwa Wilaya ya Temeke siyo nzuri kwani zinasikitisha mno, kwani
mmoja kati ya wanawake watatu wanaotumia dawa hizo ameathirika na Ukimwi
huku wa wanaume wawili kati ya wanne wameathirika na Ukimwi.
Kuhusu magonjwa mengine, amesema kama yale ya homa ya ini pia ni hatari kwa afya na huwaandama vijana hao.
Naye Mwenyekiti wa Vijana wa Wilaya ya Temeke,
Oliver Mwambope amesema, kutokana na ukweli kuwa vijana hujiingiza
kwenye wimbi la matumizi ya dawa za kulevya, chama chake kimeweka
utaratibu maalumu wa kupambana na tabia zote hatarishi zikiwamo zile za
matumizi ya dawa hizo.
Mara kwa mara tumekuwa tukiendesha kampeni za kupambana dawa za kulevya pamoja na tabia nyingine hatarishi.
Pamoja na utaratibu huo, Mwampombe alisema,
hutumia hadhira hususani zinazowahusu vijana kukumbushana kuhusiana na
mapambano hayo.
Baraza la Vijana wa Temeke, hufanyika kila mwaka
mara moja likiwajumuisha wajumbe wa umoja wa vijana wa vijana kutoka
katika kata zote za majimbo ya Temeke na Kigamboni wakilenga kujadiliana
masuala mbalimbali yanayohusu mustakabali wa maendeleo yao.
No comments:
Post a Comment