Mapenzi yanachukua nafasi kubwa sana katika maisha yetu lakini
mapenzi hayahaya yanafikia hatua tya kuwadatisha baadhi ya watu. Wengi
wasiojua sarakasi zilizomo kwenye uwanja wa mapenzi wanashindwa kujua
mchezo unakwendaje na kujikuta wakilizwa wasipate ile furaha
waliyoitarajia.
Naamini
tunajua usanii uliopo katika ulimwengu wa sasa wa mapenzi. Wengi wapo
kwenye mapenzi ya kitapeli kwa kuingia kwenye uhusiano na watu ambao
hawana mapenzi ya dhati bali wanatafuta pesa.
Kutokana na kuwepo kwa mabadiliko ya teknolojia, wapo ambao wamekuwa
wakiingia kwenye uhusiano na watu ambao wako mbali. Unakuta msichana
yupo Dar, anapata namba za simu za mvulana aliye Arusha na wanaanzisha
uhusiano.
Yawezekana kweli watu hawa wakaendeleza uhusiano wao na siku moja
wakafunga ndoa na kuweka historia. Hata hivyo, baadhi wamejikuta
wakiangukia kwa matapeli huku wakishea penzi na watu wengine bila kujua.
Nasema hivyo kutokana na ushuhuda wa mmoja wa wasomaji wa safu hii
aliyejitambulisha kwa jina la Jackson ambaye alinieleza jinsi
alivyofanyiwa usanii na binti ambaye alidhani amepata kumbe amepatikana.
Hebu msikie uone jinsi mapenzi ya simu yalivyojaa ulaghai;
“Nilionana naye mara moja mjini Arusha, tukapendana. Nikachukua namba yake na yeye akachukua yangu kisha mimi nikarudi Dar.
“Kuanzia hapo tukawa tunawasiliana, alikuwa akinipa maneno matamu
sana huku akinionyesha kuwa kwenye moyo wake niko mimi tu. Nikawa
najitutumua kwa matunzo, kila wiki lazima nimtumie pesa, vocha za hapa
na pale, lengo langu aepukane na vishawishi vya wanaume wakware.
“Nilipoingiza suala la kutaka kwenda kwao ili akanitambulishe kwa
wazazi wake hapo ndipo alipoanza kunichenga. Mara simu yake haipatikani,
mara haipokelewi na nikituma meseji zikawa hazijibiwi.
“Nikaanza
kupata wasiwasi, nikalazimika kufunga safari hadi Arusha na nilipofika
nikampigia simu, alipopokea na kumwambia niko Arusha akakata na kuanzia
hapo sikumpata tena.”
Huyu ni mmoja tu kati ya wengi ambao waliyaamini mapenzi ya simu
lakini mwisho wake yakawatokea puani. Hapa ni suala la kujiaminisha tu
na huyo mtu wako ambaye mara nyingi mmekuwa mkiwasiliana kwenye simu.
Unachotakiwa kujua ni kwamba, wapenzi wengi wa kwenye ni simu ni
walaghai.
Watatumia maneno matamu kukulainisha lakini baadaye wanakugeuza
kitega uchumi. Mizinga ya hapa na pale haitakosekana na meseji za ‘bebi
sina credit’ kila siku lazima ziwepo, bado hujashtuka tu?
Sikia
msomaji wangu, sasa hivi wapo wasichana wa namna hii, anaingia kwenye
uhusiano na wewe na kuonesha anakupenda sana lakini ukiacha wewe kuna
wanaume wengine zaidi ya watatu.
Anachokifanya kila siku asubuhi anawatumia wote meseji kwamba ana
shida ya pesa. Katika watatu hao hatakosekana mmoja au wawili ambao
watatuma. Wapo wanaoendesha maisha yao kwa njia hiyo.
Sasa kwa nini ukubali kuingia kwenye cheni ya wanaume kibao
wanaomhudumia msichana mmoja ambaye anawachukulia nyie kama wajinga
wake? Yes, nasema anawachukulia kama wajinga wake kwa kuwa ameweza
kuziteka akili zenu na kuhisi mnapendwa kumbe hamna lolote, usanii
mtupu!
Nimelazimika kuiandika makala haya ili kujaribu kuwazibua masikio
baadhi ya watu si, wanaume tu bali hata wanawake. Wapo ambao sasa hivi
wako kwenye mapenzi ya kilaghai huku wakidanganywa na maneno matamu ya
kwenye simu.
Ni muda muafaka kwako sasa kuutathmini uhusiano ulionao hasa kwa wewe
ambaye uko mbali na mpenzi wako na kuangalia kweli anakupenda au
anakulaghai na kukugeuza ATM huku akiwa na wengine? Usizubae katika
hili. Hakika wajanja watakucheka!
No comments:
Post a Comment