Saturday, 4 May 2013

Wamtaka JK kutoa msimamo wa kisheria kwa Uislamu, Ukristo...........




Jukwaa wa Wakristo Tanzania limemtaka Rais Jakaya Kikwete kutoa msimamo wake kisheria ambao utaleta upatanisho kati ya waumini wa dini ya Kiislamu na Kikristo.
Jukwaa hilo limesema kauli iliyotolewa na rais juzi wakati wa sherehe za Mei Mosi, Mbeya ya kutaka Watanzania waishi kama zamani ina utata kwa sababu imetafsiriwa tofauti na baadhi ya Watanzania.
Hivi karibuni Rais Kikwete wakati akizungumza kwenye sherehe za Mei Mosi alisema Serikali bado inaendelea kuzungumza na viongozi wa dini wa pande zote na kuwaunganisha ili kuona maelewano yanarejea kama ilivyokuwa zamani na kuwataka Watanzania waendelee kuishi bila kubaguana au kuchukiana kwa dini zao.
Akizungumza jana, Mwenyekiti wa jukwaa hilo, Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu wa Kikatoli Tanzania (TEC), alisema licha ya maneno hayo kuwa mazuri lakini bado kuna utata kwa sababu baadhi ya raia wameingiwa na wasiwasi.
Alisema maeneo mengine wakristo hawali nyama kwa sababu hawataki kulazimishwa kula nyama zilizochinjwa kwa ibada za kiislamu na kwamba suala hilo siyo dogo kama wengine wanavyofikiri kwa sababu limegharimu maisha ya watu.
Alisema licha ya kuwapo kwa kauli za uchochezi wa kuwaua viongozi wa dini ya kikristo,kuchoma makanisa na mauaji ya viongozi wa kikristo bado hazijafutwa wala waliozitoa hawajakamatwa na kwamba hawajui kinachoendelea.
Mwenyekiti huyo alisema madai ya msingi ya waislamu yaliyosababisha waanzishe vurugu na mauaji hayajajibiwa na Serikali huku maswali yaliyoulizwa na wakristo kutokana na madai hayo na vurugu hizo nayo yakiwa hajayajibiwa.
Alisema licha ya kukutana na Rais Kikwete Aprili 23, mwaka huu ambaye alihimiza viongozi wa wakristo na waislamu wakutane ili kuondoa tofauti zao zisizo za kiimani lakini bado wanasubiri maelekezo toka serikalini kwani ajenda ya uvunjifu wa amani viongozi wa dini hawawezi kuizungumzia kwa sasa bila majibu ya Serikali kwa madai yaliyozua uvunjifu huo wa amani.

No comments:

Post a Comment