Monduli. Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa amepinga vikali dhana kwamba sekondari za kata zimechangia matokeo mabaya ya ufaulu kwa wanafunzi wa kidato cha nne.
Akizungumza katika semina ya wadau wa elimu wilayani Monduli juzi, Lowassa alisema anapinga kwa nguvu zote fikra hizo.
Hata hivyo, katika utafiti wa hivi karibuni wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), kwa mikoa 20, ulibaini kuwa sekondari nyingi za kata zinafanya vibaya kwa sababu mbalimbali.
Unaainisha sababu hizo kuwa ni kukosa walimu, wanafunzi hawapati chakula, maabara, kukosekana vitabu vya ziada na kiada na wakati mwingine hulazimika kutembea umbali mrefu kwenye mazingira hatarishi.
“Napinga kwa nguvu zangu zote dhana hiyo, hizo shule za kata ni mkombozi wa elimu kwa wananchi, zikiwezeshwa kwa walimu, nyumba za walimu, vitabu na vitendea kazi vingine, kwa kweli naamini zitakuwa bora kuliko hata za binafsi,” alisema Lowassa na kuongeza:
“Hizo shule ni kielelezo cha usawa kwa elimu kwa Mtanzania, ni mkombozi kwa mtoto wa mwananchi kule kijijini.”
Alisema kutapakaa kwa shule hizo kila kata nchini, ni uthibitisho wa kielelezo cha usawa wa elimu.
Lowassa ndiye aliyesimamia ujenzi wa sekondari hizo za kata wakati akiwa Waziri Mkuu. Semina hiyo ya siku mbili inajadili mwenendo wa elimuWilaya ya Monduli na Lowassa alisema vikao vya mara kwa mara sasa vinatosha, kinachotakiwa ni utekelezaji.
No comments:
Post a Comment