Ni vyema sasa Katiba Mpya ikaweka kufuli kwa mambo makubwa yanayogusa Katiba ya nchi ili kanuni za Bunge zisitumike kwa matakwa ya mtu mmoja
Wasomi na Wanaharakati wamesema wangependa kuona Katiba Mpya ikipunguza nguvu ya Kiti cha Spika wa Bunge ili kutenda haki, wakieleza kuwa inavyoonekana, kiti hicho sasa kinaongoza kwa mabavu na upendeleo.
Wakitolea mfano wa tukio la hivi karibuni la wabunge wa Chadema kusimamishwa kuhudhuria vikao vya Bunge kwa siku tano, wamesema, hawaamini kama hatua hiyo ilifikiwa kwa haki.
Aprili 17 mwaka huu Naibu Spika Job Ndugai aliamuru askari wa Bunge wawatoe nje ya ukumbi wabunge sita wa Chadema ambao waliwazuia askari hao kumtoa nje Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu.
Wabunge wengine waliotolewa nje na kuzuiwa kuhudhuria vikao vya Bunge kwa sita tano Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini), Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini), Highness Kiwia (Ilemela), Ezekiah Wenje ( Nyamagana), na Godbless Lema wa Arusha Mjini.
Uamuzi huo wa Naibu Spika licha ya kupingwa na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni Freeman Mbowe, umeungwa mkono na Spika Anne Makinda aliyetumia kanuni ya 2(2) na 5(1). Akitumia kanuni hizo, Spika Makinda anasema, “Uamuzi uliofanywa na Ndugai ni halali na utaingizwa kwenye kitabu cha maamuzi ya Spika.”
Jukata wapinga
Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Deus Kibamba anasema, Nguvu za Spika katika Bunge ni kubwa mno, hivyo katiba inapaswa kuangalia upya suala hilo na kulifanyia marekebisho.
Anasema nguvu ya Spika ni kubwa kiasi kwamba hata Kamati ya Uongozi na Maadili ya Bunge, haiwezi kumdhibiti kwa kuwa yeye ndiye Mwenyekiti na Naibu wake ni Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo.
“Ukifuatilia kwa makini, Kiti cha Spika hakikutumia kanuni hata moja. Uamuzi ule ulitungwa tu na Naibu Spika Job Ndugai na kisha kupata baraka za Spika Makinda,” anasema Kibamba na kuongeza;
Wingi wa wabunge wa CCM, unachangia kiti cha spika kupindisha na kukiuka baadhi ya kanuni za Bunge katika hali inayoonyesha kutaka kuubinya upinzani.
“Ni vyema sasa Katiba Mpya ikaweka kufuli kwa mambo makubwa yanayogusa Katiba ya nchi ili kanuni za Bunge zisitumike kwa matakwa ya mtu mmoja.”
Kibamba anasisitiza kuwa Katiba ijayo itamke wazi kuwa ni marufuku kwa chombo chochote kubadilisha ibara yoyote ya Katiba kwa manufaa yao, lakini pia mgombea binafsi wa Kiti cha Spika aruhusiwe.
No comments:
Post a Comment