Thursday 19 September 2013

ANAKULIZA KILA MARA LAKINI UNASHINDA KUMUACHA?

Haya karibuni tena kwenye ‘mambo yetu yale’ ya malavudave, si unajua bila mapenzi hakuna maisha! Huo ndio ukweli, huwezi kuishi kama jiwe au mti. Raha ya maisha ni kuwa na mwenzi, mpenzi wa kumpenda na kukupenda ki ukweli na sio kujaribu au kuzuga.

Kwa wale walio katika mapenzi matamu na ya kweli watakubaliana na mimi kuwa mapenzi yenye amani na masikilizano ni kama ‘ka paradiso’ kadogo ndani ya ulimwengu huu mkubwa uliojaa vituko! Wakati mwingine unaweza hata kujikuta umeshiba bila kula, eti kwa sababu tu umemuona mpenzio au kuwa nae karibu tu yaani yeye kwako ndo’ mambo yote, yeye ndio kila kitu! Raha ilioje!
Wakati wengine wakiishi kwa raha katika maisha yao ya kimapenzi, wapo wengine wanaoishi na wapenzi wao huku mioyo yao ikiwa imesinyaa! Kila siku ni karaha na vituko vya makusudi kutoka kwa wapenzi wao japo wanawapenda sana na kuonesha mapenzi yao yote. Kila siku ni maumivu na simanzi ya moyo isiyojulikana mwisho wake.
Lakini pamoja na karaha, vituko na dharau zinazofanywa na wale tuwapendao bado kuna wale wenzangu na mimi utakaowasikia wakisema “Ah! Nitavumilia tu, labda atabadilika na nafikiri sitoweza kumuacha kwa kuwa nampenda sana!”
Jamani, huenda nikawa na msimamo tofauti kidogo, lakini mimi naamini kuwa mapenzi ya kweli ni pamoja na kumsikiliza mwenzio na kuheshimu hisia zake, hasa katika mambo yanayofaa. Tofauti na hapo, tabia ya kutokuwa msikivu, kutojali na kutokuwa mwepesi kubadilika ni dalili tosha ya kutokuwepo kwa upendo wa kweli na wa dhati. Mapenzi nijuavyo mimi ni kupenda, kupendwa, kusikizana na kuheshimiana na si vinginevyo!
Hata hivyo naomba nichukue nafasi hii kuwapa pole wale wote wanokwazwa na wapenzi wao kwa namna moja au nyingine kwa sababu mbalimbali kama vile usaliti katika mapenzi, ulevi, ujeuri, kutojali, vipigo na ubabe na mengineyo mengi.
Na pia nafahamu kuwa wakati mwingine unajikuta katika wakati mgumu wa kuamua hatma ya uhusiano wako na mpenzio kwa kuwa unahisi unampenda sana na kwamba hauko tayari kumkosa maishani. Labda tubadilishane mawazo, kama wewe ni mmoja wapo kati ya wanaokabiliwa na hali hii. Hebu jaribu kupitia dondoo zifuatazo
Mueleze jinsi unavyokwazika
Ni vizuri kabla hujaanza kulalamika kwa watu wa pembeni, hakikisha unamwambia ukweli mwenzi wako juu ya tabia yake na kumueleza ni jinsi gani unaumizwa mno na tabia hiyo.Lakini hakikisha unaongea nae katika hali ya upendo na sio kuporomosha lawama na kubwatuka hovyo, la sivyo atakugeuzia kibao na mtakosana zaidi.
Ana dalili ya kubadilika?
Kwa mpenzi anayeonesha angalau kubadilika ni heri kwako, lakini kwa wale “sugu” ambao wanaendeleza tabia zao hata mwaka mzima na kuwa hodari sana wa “samahani honey, si unajua binadamu hukosea na kujisahau, nisamehe mpenzi.” Hivi hii ni samahani gani wakati unarudia makosa yale yale kila kukicha, mpenzi wako akueleweje kama sio kumdharau. Ukiwa na mtu wa namna hii, mtazame vizuri kisha uamue!
Tabia yake inavumilika?
Jamani kuna mambo mengine madogo madogo yanaweza kuvumilika kwa kuwa huenda “sio ishu sana.” Lakini kuna tabia nyingine huna haja ya kuzifumbia macho na kujiongopea kuzivumilia. Kwa mfano tabia ya vipigo kila siku, utavumilia mpaka utakapotolewa macho au unyofolewe na roho yenyewe kabisa au? Mpenzi Malaya, utamvumilia mpaka pale atakapokuletea Ukimwi uhangaike nao? Sidhani kama ni busara kuvumilia haya, usikubali kabisa kupelekwa pelekwa na hiyo hisia yako ya “lakini nampensa sana!” Hebu jiangalie vizuri.
Omba ushauri
Wakati mwingine ni vyema sana ukawaomba watu ushauri juu ya nini ufanye unapokabiliwa na msongo wa mawazo unaotokana na kero za mpenzi wako. Kwa wanandoa wanaweza kuwahusisha wazee na wakati mwingine hata vyombo vya sheria. Usikubali kunyamaza na “kumezea” matatizo uliyo nayo, utakufa kihoro buree! Waombe ushauri wale unaowaamini huenda wakakuonesha njia.
Jifunze kwa wengine
Jiulize, hivi ni wangapi unaowafahamu na wengine kusikia habari zao, ambao waliwahi kupenda kama wewe lakini kutokana na manyanyaso na kutosikilizana wameachana na wapenzi wao, na sasa wanaishi maisha mengine matam na wapenzi wao wapya, kwanini usiwe wewe?
Ondokana na “siwezi kuishi bila yeye”
Kumbuka kauli ya “siwezi kuishi bila yeye” ni minyororo na kufuli nzito unayojifungia nayo katika jela yako wewe mwenyewe. Hebu jaribu kupigana kiume na mawazo haya na ujiweke huru. Hakuna anayeshikilia pumzi ya mwingine!
Kuwa jasiri fanya maamuzi
Pamoja na yote, ukweli unabaki palepale kwamba kuamua, “kummwaga” mtu unayempenda si kazi ndogo, lakini inafikia mahali inakuwa haina jinsi inakubidi. Uwe jasiri ili uondokane na maisha ya “roho juu juu” kila siku! Potelea mbali ili mradi upate uhuru wa nafsi.
Amini wa kwako aja!
Amini kuwa huenda Mungu hakukupangia ufurahi maisha na huyo uliye naye sasa kwa kuwa yule wako “original” bado yu njiani na kusahau machungu yaliyopita Inshaallah!

No comments:

Post a Comment