Thursday, 6 February 2014

Unafahamu ndoa ni sawa na kumiliki gari?

Kichwa cha habari hapo juu kinazungumza kila kitu kuhusu uhusiano wa kimapenzi au maisha ya ndoa. Ni sawa na mtu anayemiliki gari. Kwa wale ambao wamezoea kupanda magari ya usafiri wa jumuia, yaani daladala, hawawezi kujua nini maana ya kumiliki gari.


Wengi wangependa kumiliki magari, lakini wanashindwa gharama, kwanza za kulinunua na pili katika kulihudumia. Baadhi ya watu husema gari ni sawa na nyumba ya madeni, kila siku utahitaji fedha katika kulihudumia.

Katika barabara yenye miamba ya uhusiano wa mapenzi, ni lazima uwe na gari imara na lenye uwezo wa kuhimili misukosuko ya safari, hii ni zaidi ya huduma nyingine kama matairi mazuri, ubadilishaji wa mafuta ya kulainisha vyuma na vitu vingine vinavyohusiana na hivyo.

Uhusiano wa kimapenzi unahitaji kujali na kuthamini kutoka kwa kila mshiriki. Kila mmoja anawajibika katika kuhakikisha gari linakuwa tayari kwa safari wakati wowote, limejaa mafuta, limefanyiwa ‘service’

 nzuri, bima yake ipo sawa, vifaa vyote vinavyotakiwa ndani yake, kama jeki, ‘fire extinguisher’ navyo vipo, ili wakati wowote likianza mwendo, asije akatokea trafiki wa kulipiga mkono na kulitoa kasoro.

Inapotokea bahati mbaya kwamba mmoja wa wapenzi, awe baba au mama, anaona kama gari hilo halimuhusu, kwamba yupo mwenye wajibu wa kulitunza, kulihudumia na kulijali, ni lazima tatizo litatokea. Ili gari liwe kamilifu linahitaji baadhi ya vitu muhimu vifuatavyo.
Fedha
Ingawa mara nyingi watu hupenda kutofautisha vitu hivi, lakini ukweli ni kwamba ni vigumu sana uhusiano au ndoa kuhimili vishindo bila uwepo wa fedha. Si fedha kwa maana ya nyingi, isipokuwa zile kidogo zinazoweza kukidhi mahitaji muhimu ndani ya uhusiano wenu.


Baba anaweza kuwa asiwe tajiri, lakini angalau awe na uwezo wa kurekebisha masuala muhimu yanayomhusu mama, ambaye naye anatakiwa kuwa tayari kupokea chochote kulingana na kipato cha mwenzake. Hali kama hii pia inaweza kuwepo kwa mama, ingawa mfumo dume unawatoa wanawake katika jukumu la wenye kuwajibika katika gharama za maisha ya kila siku ya walio katika uhusiano.

Inapotokea fedha haziwezi kukidhi mahitaji muhimu ya mke au mwenza, ni wakati ambao wengine huamua kuzitafuta kwa kutoka nje ya uhusiano wao. Ni kweli, anaweza kuwa anampenda mwenza wake, lakini pia anayo mahitaji mengine ambayo hawezi kuyapata kwa aliyenaye, vipi atashindwa ‘kuchepuka’ ili ayapate?

Uzoefu hata hivyo, unaonesha kuwa uwepo wa fedha nyingi katika familia nyingi, husababisha matatizo. Pesa huanza kuleta migogoro, mama ataona baba anatumia vibaya fedha zake kwa kutafuta wanawake wa nje.

Usalama

Penzi, kama lilivyo gari, linahitaji usalama. Ni lazima uwepo ulinzi wa maana kwa ajili ya kulilinda na huyu ni lazima awe wewe au mimi.


Kila mmoja anao wajibu wa kuhakikisha gari halisogelewi, siyo tu na wezi, bali hata vumbi, kwa sababu linaweza kuingia ndani na kulifanya liwe chafu.


Mara kadhaa penzi linaonekana kuwa ni mchanganyiko wa furaha na maumivu. Kama mdau wa uhusiano, ni lazima uweke katika hali ya uwiano wa moyo na akili. Kipi kinahitaji moyo na kipi kinahitaji akili.

Wakati mwingine mwenza wako anaweza kuwa mwenye kuvutiwa na vitu ambavyo wewe huvutiwi navyo. Kama utaweka moyo katika suala kama hili, waweza kudhani kuwa kwa vyovyote yupo mtu ambaye anashiriki naye kimapenzi katika hayo mambo anayoyapenda, lakini ukiwekeza akili, ni rahisi kutambua kwamba kama binadamu, tofauti ya kupenda vitu visivyofanana ni jambo la kawaida.

No comments:

Post a Comment