Friday, 26 April 2013

Chui amjeruhi mfugaji sehemu ya makalio.....



Mimi nilimwona huyu ndugu yangu akiminyana na chui ila sikujua kama ni huyo mnyama na kuhisi ni kama kawaida yetu tukiwa katika malisho mara unaenda huku mara kule tena mbio, wakati anapiga kelele na kumfuata nikaona ni chui,”


Pangani. Mfugaji wa Jamii ya Kimang’ati katika Wilaya ya Pangani, Ndoyo Ikejo amenusurika kuliwa na chui katika jitihada zake za kumnasua ndama wake kutoka mdomoni mwa mnyama huyo na kisha kumgeukiwa yeye na kumtafuna mguu na sehemu ya makalio yake.
Hivi karibuni Mkuu wa Wilaya ya Pangani. Hafsa Mtassiwa aliendesha operesheni ya kuwataka wafugaji waliovamia wilaya hiyo, kuhama na mifugo yao au kupunguza idadi ya ng’ombe zao na kuondosha kitisho cha mapigano baina ya wakulima na wafugaji hao.
Wakizungumza na gazeti hili wakiwa katika Hospitali ya Pangani, ndugu wa mhanga huyo walisema, Ikejo alikuwa katika uchungaji wake wa kawaida na alipokuwa Msitu wa Mkalamo katika Mto Mkwaja alimwona chui akiwa katikati ya ng’ombe wake.
Festo Moris ambaye wakati wa tukio alikuwa jirani na mto huo, alisema alimwona Ikejo akisukumana na chui bila ya yeye kujua kama ni chui na kudhani ni moja ya ng’ombe wake.
“Mimi nilimwona huyu ndugu yangu akiminyana na chui ila sikujua kama ni huyo mnyama na kuhisi ni kama kawaida yetu tukiwa katika malisho mara unaenda huku mara kule tena mbio, wakati anapiga kelele na kumfuata nikaona ni chui,” alisema Moris.
Moris alisema tukio hilo ni la kwanza kutokea Pangani na limewashtua, kwani hakujawahi kuripotiwa matukio hayo na hivyo kutakiwa kuchukua tahadhari na kuacha kuwapeleka ng’ombe katika malisho na mtu akiwa peke yake.
Akizungumzia tukio hilo,Mkazi wa Kijiji cha Mkalamo, Juma Hemed alisema mfugaji huyo alinusurika kuliwa na chui baada ya kumzuia asile ndama wake na ndipo alipomgeukia yeye na kumtafuna mguu na sehemu ya kulia ya makalio yake.
Alisema ilikuwa bahati nzuri kwake kwani angeweza kumla mwili wake wote, ila jitihada zake za kuminyana akiwa na silaha za jadi pamoja na kelele ziliweza kumsaidia na hivyo kuwashauri wafugaji hao kulisha mifugo yao wakiwa vikundi.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Diwani wa Pangani Magharibi, John Semkande alisema lilitokea saa 5 asubuhi wakati mfugaji huyo akiwa katika malisho ya mifugo yake na kupelekwa katika hospitali ya Wilaya.
Alisema kijana huyo hali yake inaendelea vizuri ila familia yake imemchukua na kumpeleka katika matibabu mengine zaidi na kuwataka wafugaji hao  kuacha kupeleka mifugo karibu na hifadhi za mbuga za Taifa.
Alisema Wilaya ya Pangani iliyoko  Mbuga ya Wanyama ya Saadani, imekuwa na wanyama wengi na hivyo kuwataka wananchi kuwa mbali zaidi na mbuga hiyo kwani wanaweza kupatwa na madhara zaidi.

No comments:

Post a Comment