SHULE ya Sekondari ya Ilboru, jijini Arusha imefungwa kwa muda usiojulikana kuanzia leo baada ya kuwepo hofu ya kuchomwa moto.
Uchunguzi wa madai ya shule hiyo
kuchomwa moto, unaendelea kufanywa huku ikielezwa kwamba wanafunzi wanne
wanahojiwa na polisi wilayani Arumeru wasaidie kubaini ukweli juu ya
madai hayo.
Wanafunzi wengine 10 inadaiwa wamepewa barua za kusimamishwa shule kwa siku kadhaa wakihusishwa na suala hilo.
Tangazo la kufunga shule hiyo lilitolewa
ghafla leo asubuhi na Mkuu wa Shule, Julius Shila baada ya kushauriana
na bodi yake, huku polisi wa kawaida wakifanya doria kudhibiti vurugu
zozote ambazo zingeweza kutokea.
Ingawa Mkuu wa Shule, Shila hakutaka
kuzungumzia suala hilo, Kaimu Ofisa Elimu wa Mkoa, Sifael Mollel,
alisema uchunguzi wa madai hayo unaendelea katika kipindi hiki ambacho
wanafunzi wamepewa likizo.
Alisema kuwepo kwa hofu hiyo na wasiwasi
wa kuzuka vurugu ndiko kulikosababisha shule ifungwe kwa muda licha ya
kwamba walikuwa hawajamaliza mitihani.
“Uongozi umeamua wanafunzi warudishwe
nyumbani kutokana na hofu ya kuchomwa moto shule, wanafunzi walikuwa
wakifanya mitihani kabla ya kuanza likizo fupi lakini uwepo tishio hilo
na kuzuka kwa vurugu, ilionekana ni vema ikafungwa,” amesema.
Alisema kwa kawaida likizo fupi ni ya
siku 10 lakini kwa tukio hili wanafunzi hao wamepewa maelekezo ya kwenda
kuonana na wakuu wa wilaya zao kwa udahili kabla ya kurejea tena
shuleni.
Akizungumzia vitisho vya moto, alisema
wanafunzi hao waliwasilisha barua ofisini kwake wakitoa madai kuwa
baadhi ya walimu walikuwa wanataka kuchoma moto shule hiyo.
Alisema polisi walienda kufanya uchunguzi Ijumaa ambapo walinusa harufu ya petroli iliyokuwa imemwagwa jirani na bweni.
Hata hivyo Kaimu Ofisa Elimu huyo
hakutawataja wanafunzi ambao wanahojiwa na polisi wala wanafunzi 10
ambao wamesimamishwa kwa siku 21.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Liberatus
Sabas, alikiri polisi kuwepo shuleni hapo wakati tangazo la kufungwa
shule likitolewa akasema hiyo ilikuwa ni kwa sababu ya kuimarisha
usalama.
Kwa mujibu wa tangazo hilo, wanafunzi wote watatakiwa kurejea shuleni hapo baada ya kudahiliwa na wakuu wa wilaya zao.
No comments:
Post a Comment