MWALIMU wa Shule ya Sekondari Mwembeni mkoani Mara, amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya, akikabiliwa na mashitaka mawili ya kuwabaka wanafunzi kwa nyakati tofauti.
Andrew Shadrack (26) ambaye aliwahi
kufundisha masomo ya Kingereza na dini katika Shule ya Sekondari ya
Montfort wilayani Mbarali mkoani Mbeya alifikishwa mbele ya Hakimu
Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Kamago Minja.
Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Luchagula Mazoya alidai mwalimu huyo alitenda makosa hayo Septemba 13 mwaka huu usiku.
Katika shitaka la kwanza, Mazoya alidai
saa 3:30 usiku wa tarehe hiyo, Mwalimu Shadrack alimbaka kwa nguvu
mwanafunzi wa kidato cha nne katika Shule ya Montfort mwenye umri wa
miaka 17, aliyekuwa akijisomea baada ya kumwita na kumpeleka gizani.
Alidai katika shitaka lingine, siku hiyo
Septemba 13 saa 4:00 ikiwa ni nusu saa kupita baada ya tukio la kwanza,
Mwalimu Shadrack alimbaka mwanafunzi mwingine wa kidato cha nne shuleni
hapo aliye na umri wa miaka 18, aliyemwita kutoka katika bweni
alimokuwa amelala.
Alidai mbinu iliyotumiwa na mshitakiwa
kwa wanafunzi hao wote, licha ya kutumia nguvu, alikuwa akiwaahidi mambo
mbalimbali, ikiwemo kuwasaidia kimasomo, akiwaeleza kuwa anataraji
kurudi shuleni hapo na kushika wadhifa wa ukuu wa shule.
Kutokana na kile kilichodaiwa ni uzito
wa mashitaka husika, upande wa walalamikaji uliiomba Mahakama,
kutoruhusu dhamana kwa mshitakiwa.
Hakimu Minja alikubaliana na maombi hayo
na kufunga dhamana, hivyo mwalimu huyo ataendelea kukaa rumande hadi
Septemba 18 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment