Figo ni ugonjwa ambao unaonekana kuwasumbua watu wengi nchini.
Baada ya siri ya ugonjwa uliosababisha kifo cha aliyekuwa Waziri
wa fedha, Dk William Mgimwa ikidumu kwa siku kadhaa, baadaye Serikali
ilisema kilichosababisha kifo chake ni ugonjwa wa figo.
Dk Mgimwa alifariki Januari Mosi, mwaka huu katika
Hospitali ya Kloof Medi Clinic, Pretoria nchini Afrika Kusini alikokuwa
amelazwa.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk Servacius
Likwelile uliutaja ugonjwa huo mbele ya waombolezaji waliofika kuuaga
mwili wake kwenye Viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.
Likwelile alisema: “Marehemu Mgimwa alikwenda
Hospitali ya Kloof Medi Clinic, Afrika Kusini Novemba 3, mwaka 2013 kwa
ajili ya uchunguzi wa kawaida wa afya yake. Baada ya uchunguzi,
madaktari walimshauri alazwe kwa uangalizi zaidi na matibabu na kwamba
aliendelea na matibabu ya figo hadi kifo chake.”
Kwa nini figo hushindwa kufanya kazi?
Figo ni viungo vilivyomo ndani ya mwili vyenye
kazi ya kuchuja uchafu uliomo kwenye damu. Vinahusika pia na uratibu wa
shinikizo la damu, madini yenye umeme ndani ya damu na uzalishaji wa
chembe nyekundu za damu.
Kati ya sababu nyingi za figo kushindwa kufanya
kazi ni shinikizo la juu la damu na ugonjwa wa kisukari. Kwa takwimu
inaonyesha kuwa zaidi ya nusu ya watu wazima wenye matatizo ya figo
husababishwa na magonjwa hayo.
Kwa kisukari; kama haujatibiwa ipasavyo, sukari
itajijenga ndani ya damu na ikiwa nyingi huharibu seli hivyo hupunguza
uwezo wa figo kuchuja uchafu.
Kuna aina mbili za kisukari, kwanza kisukari
ambacho mwili unashindwa kuzalisha tezi inayomeng’enya sukari kwenye
damu (insulin). Kisukari cha pili ni pale mwili unaposhindwa kutumia
vizuri insulin inayozalishwa.
Kwa tatizo la shinikizo la juu la damu; ni pale
kunapokuwa na shinikizo kubwa la damu kuliko ukubwa wa mishipa yake.
Kama shinikizo hilo litaongezeka litasabisha ugonjwa wa moyo, mshtuko na
ugonjwa sugu wa figo.
Sababu nyingine ni kuharibika kwa seli
zinazohusika na uchujaji wa uchafu hali inayosababisha kupungua kwa
mkojo, kutokutolewa kwa protini katika mkojo na kuvimba kwa mikono na
miguu.
Nyingine ni magonjwa ya kurithi kama vile
‘Polycystic’ yaani vivimbe kutokea ndani ya figo hivyo kushindwa
kufanya kazi. Magonjwa kama haya siyo ya kawaida lakini huanza wakati
mtoto akiwa bado tumboni.
No comments:
Post a Comment