Monday, 13 January 2014

Israel yamkumbuka Ariel Sharon

Israel imetoa heshima kwa waziri mkuu wa zamani Ariel Sharon katika moja kati ya ibada mbili za kumuaga kiongozi huyo anaesifika kuwa shujaa wa kivita nyumbani, lakini anaeonekana kama mhalifu wa kivita kwa wengi katika mataifa ya Kiarabu. Makamu wa rais wa Marekani Joe Biden alishiriki shughuli ya kumuaga Sharon mbele ya bunge la Israel, na alitarajiwa kuhudhuria mazishi yake ambayo yanafanyika shambani kwake kusini mwa Israel.

Sharon alifariki  Jumamosi akiwa na umri wa miaka 85, baada ya kuwa mahtuti kwa miaka minane kutokana na ugonjwa wa kiharusi. Kifo chake kimeamsha tena mjadala juu ya urithi wake, huku wapinzani wake wakilaani tabia yake ya kikatili katika operesheni za kijeshi, wakati marafiki zake wakimsifu kama mpanga mikakati aliyeishangaza dunia mwaka 2005 kwa kuwaondoa wanajeshi wa Israel na walowezi kutoka ukanda wa Gaza.

No comments:

Post a Comment